Mafundi minara 30 wafariki dunia mbugani

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:09 AM Oct 09 2024
Minara.
Picha: Mtandao
Minara.

MAFUNDI wa Minara Tanzania (Tanzania Riggers), wameomba kupatiwa vifaa vya kufanyia kazi, kutokana na kukutana na mazingira hatarishi wanapokwenda kufanya kazi porini, mbugani na kusababisha vifo zaidi ya 30.

Pia, wameiomba serikali na kampuni zinazojihusisha na utoaji wa huduma za mawasiliano ziwape mikataba na bima za afya kwa sababu kazi wanayofanya ni ya mionzi, wanaweza kupata madhara wakati wowote na familia zao zikabaki hazina msaada.

Mwenyekiti wa Tanzania Riggers, Eliud Gobeka, alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu chama hicho na mikakati ya kukiimarisha.

Alisema wamejikuta wanafanya kazi katika mazingira hayo kwa sababu shughuli zote kwa sasa zinajengwa vijijini kwenye wanyama wakali na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

"Tunakutana na hali hii kwa sababu ya kukosa vitendea kazi hatupewi magari tunatumia usafiri wa bodaboda, hivyo tunaomba kampuni zote hasa Osha, Gravity na HEC walione hili," alisema Gobeka.

Alisema mazingira hayo hatarishi yamesababisha vifo vya vijana zaidi ya 30 tangu walivyoanza kazi ya mawasiliano zaidi ya miaka 20, wanaomba wapewa fedha na mafunzo kwa wanachama hao ili kuboresha utendaji kazi wao na kuondoa tatizo hilo.

"Kazi tunazozifanya haziendeni na kipato tunachokipata, tunatamani kampuni tunazofanya nazo kazi zitambue kipato chetu na kazi tunayoifanya ni hatarishi, kwa mfano mnara wa mita 50 tunajenga kwa Sh. milioni 2.3 kiufundi hii haijakaa sawa."

"Tunaomba kampuni zote za mawasiliano, kiwango cha fedha tutakachokubaliana watulipe chote sio zitupe kianzio na ndiyo maana tunaomba mikataba ili tuweze kupata sehemu ya kuwashtaki pindi tunapopata changamoto za malipo," alisema. 

Pia, alisema wameanzisha chama hicho chenye wanachama zaidi ya 500 kwa ajili ya kutetea haki zao kutokana na baadhi za kampuni kuwadhulumu fedha na kushindwa kujua waanzie wapi kuzishtaki, kwa sasa watafanya hivyo kwa sababu wameshasajili chama hicho.

Katibu wa chama hicho, Baraka Urio, aliiomba Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwawezesha vijana kupata mafunzo na vifaa vya kufanyia kazi ili kuleta ufanisi katika kazi zao.

Alisema baadhi ya kazi wanazofanya ni kujenga minara mipya, nguzo za umeme, kusafisha vioo kwenye majengo marefu, kujenga magodauni marefu na kuchomelea.