Mawaziri watoka ofisini wafuata wananchi mikoani

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:18 AM Oct 09 2024
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi
Picha:Mtandao
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi

NI siku 23 tangu mawaziri kuanza kukagua miradi hasa kwenye sekta nne mahsusi kwa kuangalia thamani ya fedha, kutoa maelekezo na kuzungumza na wananchi.

Mawaziri 11 wameonekana kwenye baadhi ya mikoa wakikagua miradi ya sekta ya maji, afya, elimu na barabara ambao hawawajibiki kwenye wizara zinazohusika na huduma hizo, huku katika hotuba zao wakieleza kuwa wanafanyakazi hiyo kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ni mtindo unaoendana na kuhamasisha wananchi kwa maneno na kushiriki kwa vitendo, wakiwa katika mavazi ya kikazi zaidi badala ya suti.

Mawaziri na mikoa ambayo wanafanya ziara  kwenye mabano ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (Dodoma), Waziri wa Viwanda na Biashara,  Dk. Seleman Jafo (Lindi), Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi (Mbeya).

 Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi (Shinyanga), Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (Geita).

Wengine ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda (Njombe), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (Mara), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax (Mtwara) na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro (Kagera).

ULEGA 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akikagua na kuzindua miradi mkoani Iringa katika shule ya sekondari Ifunda,Kiwere,Pawaga na Mboliboli amesema serikali imepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule kila mahali nchini.

Aidha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Willium Lukuvi, juzi alianza ziara ya kutembelea vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu, ikiwa ni kufafanua zaidi 4R za Rais Samia.

 Kinachotafsiriwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia kwa wateule wake kutoka ofisini na kuzunguka kwa wananchi na kukagua miradi ya maendeleo.

Ni mfumo ambao hata yeye (Rais), anautumia kwa kofia zake mbili Urais na Uenyekiti wa CCM Taifa ambao kwa kiasi kikubwa tangu aingie madarakani anaufanya na kwa viongozi wake wa chama kukagua na kutoa maelekezo kwa serikali.

MASAUNI

Waziri Masauni akiwa mkoani Dodoma miongoni mwa miradi aliyokagua na kushiriki kuchimba msingi ni ujenzi wa vyumba vya madarasa, shule mpya ya sekondari Mnenia Halmashauri ya Kondoa Vijijini.

Akizungumza na wananchi, Masauni alisema “Si rahisi kwa Rais, Makamu na Waziri Mkuu kupita kwenye hii miradi kwenye kata zote kuona kama imekwenda kwa mujibu wa matarajio ya serikali, je, imesaidia kuondoa kero za wananchi kama serikali inavyotaka, ndio maana tumetumwa sisi kuikagua.”

JAFO

Mkoani Lindi, Waziri Jafo alifanya ukaguzi wa miradi kwa kaulimbiu ‘Rais Samia na Maendeleo Wasikie na Waone’.

Miongoni mwa miradi aliyotembelea na kuweka jiwe la msingi ni ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Chiwindi Wilaya ya Nachingwea, mradi wa maji Naipanga na mradi wa barabara Mipingo, yenye urefu wa kilometa 0.78, Wilaya ya Ruangwa inayojengwa chini ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya Lionja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

KABUDI

Akiwa mkoani Mbeya, Waziri Kabudi aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kyela kukamilisha haraka ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Sama, ili kuwapunguzia kero ya kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni.

Alisema lengo la serikali ni kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wote bila kujali hali zao huku akisisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto kwa mujibu wa sheria za nchi.

 MAVUNDE

Waziri Mavunde ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa barabara ya Stendi ya Mabasi ya Kahumo yenye urefu wa kilomita moja kwa kiwango cha lami nyepesi wilayani Chato mkoani Geita na anaendelea ukaguzi huo pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mikutano ya hadhara.

 MKENDA

Mkoani Njombe, Waziri Mkenda amezindua Kituo cha Afya Makoga na kuwaasa wananchi Wanging'ombe kukitunza kwa kuwa kinatoa huduma bora za afya daraja la kwanza.

 SIMBACHAWENE

Waziri Simbachawene, aliwataka viongozi wa Mkoa wa Mara kutekeleza miradi ya maendeleo kwa usahihi ili idumu kwa muda mrefu na kutumika kikamilifu na wananchi.

Akizindua mradi wa Zahanati ya Getarungu wilayani Serengeti uliofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Simbachawene aliridhishwa na utekelezaji wake na kutaka halmashauri za mkoa huo kuiga utekelezaji wa namna hiyo.

 NDEJEMBI

Waziri Ndejembi akiwa Shinyanga, alikagua mradi wa ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Ntobo na ujenzi wa Kituo cha Afya Segesena kutoa mwezi mmoja kituo hicho kianze kufanya kazi kwa kuwa kimekamilika na kuwekewa baadhi ya vifaa tangu mwaka 2023, lakini hakijaanza huduma kwa wananchi. 

 TAX

Waziri Tax alieleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa shule za sekondari katika Manispaa ya Mtwara - Mikindani na Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, na kutaka ujenzi huo uzingatie ubora na thamani ya fedha.

 Mtindo huo uliwahi kutumiwa na Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa wakati alipoanzisha ujenzi wa sekondari za kata.