Morocco: Hakuna wa kuizuia Stars kwenda AFCON

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:25 AM Oct 09 2024
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Picha:Mtandao
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

WAKATI kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kiliondoka nchini jana kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kucheza mchezo wa tatu wa Kundi H, kwa ajili ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, Kaimu Kocha Mkuu, Suleiman Hemed Morocco, amesema wanakwenda kupambana ili kupata ushindi kwani hakuna wa kuwazuia kufuzu fainali hizo.

Akizungumza kabla ya kupaa na ndege maalum ya serikali, iliyotolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Morocco alisema wanafahamu kuwa wanakwenda kucheza mechi ngumu, lakini wamejiandaa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo.

Stars itajitupa kwenye Uwanja wa Stade des Martys jijini Kinshasa, kucheza na Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kesho saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Morocco alisema kwa sasa Stars inaweza kucheza na timu yoyote barani Afrika na kufanya vizuri kutokana na kuwa na wachezaji vijana, wenye uwezo mkubwa wakichanganyika na wazoefu.

"Tunakwenda kucheza na timu nzuri, na wana mwendelezo kwenye ushindi wao, siyo rahisi haitokuwa mechi ya kitoto, lakini naamini na sisi tutakwenda kuleta upinzani ili tushinde mechi hiyo, kama tulishinda dhidi ya Guinea kwao kwa nini tusiifunge DR Congo?

"Kwa sasa timu ya taifa inaweza kucheza na timu yoyote kwa sababu tuna wachezaji wazuri, vijana waliochanga na wazoefu, tunakwenda kupambana kuhakikisha lengo letu mama la kufuzu AFCON linafanikiwa," alisema kocha huyo.

Naye beki wa kushoto wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Tshabalala' alikiri kuwa wanakwenda kucheza na timu ngumu, yenye wachezaji wengi wanaokipiga nje ya Bara la Afrika, lakini na wao hawatokuwa wanyonge kwani wana maelekezo ya kufanya waliyopewa na walimu wao.

"Tumejitahidi kupokea maelekezo ya walimu wetu kuelekea kwenye michezo yetu miwili dhidi ya DR Congo, sisi kama wachezaji tunakwenda kufuata kile tulichoelekezwa kwenye mechi hiyo, tunajua kuwa wenzetu wana wachezaji wazuri sana, wanacheza klabu kubwa nje ya Afrika, hivyo tunajua kama tunakwenda kucheza mchezo mgumu, lakini na sisi tumejiandaa kushinda ugenini," alisema.

Katika mchezo huo, Stars itamkosa mchezaji aliyeitwa kwa mara ya kwanza, Abdulrazack Hamza, ambaye ameumia nyama za paja, ikamlazimu Morocco kumwita beki wa kati wa Mashujaa FC, Ibrahim Ame, kuziba nafasi yake.

Timu hizo zitarudiana tena Oktoba 15 katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mpaka, Dar es Salaam.

Katika Kundi H, Tanzania inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne, nyuma ya DR Congo, yenye pointi sita, Ethiopia ya tatu ikiwa na pointi moja, huku Guinea ikiwa haina pointi na zote zimecheza michezo miwili.