WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema watumishi wa umma wanatakiwa kuacha tabia ya urasimu kazini mambo ambayo yanachelewesha uwekezaji.
Amesema Mkoa wa Pwani ni eneo lenye fursa ya uwekezaji hivyo mambo hayo yasipofanywa na watumishi yanawavutia wawekezaji kuwekeza kwa wingi .
Bashungwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo walioshiriki kikao kabla ya kuanza ziara ya kikazi anayoifanya katika Mkoa wa Pwani akianzia Wilaya ya Kibaha.
Akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti wa Wilaya ya Kibaha amesema Serikali inaendelea na maboresho kwenye barabara kwa kuzijenga katika kiwango cha changarawe na lami kwa kutenga fedha kupitia bajeti zake.
Pia Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage kutengeneza kwa kiwango cha changarawe barabara ya kutoka Mlandizi kwenda SGRIli iweze kupitia kwa urahisi.
Waziri huyo amesema ni vema barabara hiyo ikajengwa kwa kiwango cha changarawe wakati mchakato wa kumtafuta mkandarasi wa kujenga kwa kiwango cha lami ukiendelea kwenye barabara yenye ukubwa wa Km 23.
Vilevile amewataka wananchi wanaodai fidia kwenye barabara ya Mlandizi makofia kuwa na subira wakati suala lao likiendelea kushughulikiwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameomba Wizara ya ujenzi kusaidia ujenzi wa barabara kwenye maeneo ya uwekezaji Ili kuendelea kuwavutia wawekezaji.
"Tunaomba tusaidiwe tutakuwa na mchango kwenye ukuaji wa uchumi hapa nchini endapo barabara hizi zinazounganisha maeneo ya uwekezaji zitafanyiwa kazi kwa kujengwa kukudhi mahitaji ya wawekezaji," amesema.
Kunenge amesema Mkoa huo kwasasa una maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji 27 na kwamba kwasasa wawekezaji wanaohitaji eneo ambalo lina kila huduma muhimu ikiwemo maji, umeme na barabara kurahisisha shughuli zao.
Kadhalika Kunenge ameomba Wizara hiyo kufanya maboresho katika kiwanja cha Ndege Mafia Ili kuwezesha Ndege kubwa za watalii kutua
Mkuu huyo wa Mkoa ameishukuru Serikali kwa kutoa sh.trilion 1.3 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa huo ikiwemo ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED