Chasambi afunguka kukaa benchi Simba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:28 AM Oct 09 2024
 Ladack Chasambi
Picha: Mtandao
Ladack Chasambi

WINGA chipukizi wa Klabu ya Simba, Ladack Chasambi, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo akisema kukaa kwake benchi ni kwa sababu ya kujifunza kitu kutoka kwa wakubwa zake, akiahidi siku moja atapata namba ya kudumu, huku akiwakumbusha kuwa hakuna timu yoyote duniani ambayo mchezaji atakwenda na kupata namba kirahisi bila ya kuipambania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Chasambi aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, alisema ni kweli kama binadamu ni lazima ujisikie vibaya kukaa benchi kila mechi, lakini alidai kuwa namba siku zote ni lazima uipambanie na si kupewa kama zawadi.

Mchezaji huyo amefunguka baada ya mashabiki wengi kulalamika ni kwa nini hapati nafasi ya kucheza, badala yake Kocha Mkuu, Fadlu Davids, amekuwa akimpa zaidi nafasi Joshua Mutale.

Alisema amekuwa akisikia maneno hayo kutoka kwa mashabiki, lakini yeye binafsi anaona Mutale ni mchezaji mkubwa na mzuri zaidi ambapo yeye mwenyewe ana vitu anajifunza kutoka kwake ndani na nje ya uwanja.

"Ushindani na nafasi ni mkubwa sana Simba, na hapa tu popote kwenye klabu za mpira, haijalishi sijui utoke Simba uende wapi, kote huko, lazima unapoenda ukapiganie namba, wala si vitu vigeni ni vya kawaida tu.

"Nimekuwa nikisikia suala la Mutale, vitu vinaongeleka na navisikia, kwa upande wangu mimi naona Joshua ni mchezaji mzuri sana na mwenye uzoefu mkubwa, anacheza kwa kuipambania Simba na ndiyo imemsajili, na hata nikimuungalia siyo kama anacheza vibaya, anacheza vema na mimi nina vitu vya kujifunza kutoka kwake, soka ni nidhamu," alisema Chasambi.

Kuhusu kama anajisikia vibaya kukaa benchi, winga huyo alikiri kuwa kama binadamu ni lazima ajisikie hivyo na hiyo ndiyo itakuwa inamuongezea chachu ya kufanya vizuri zaidi uwanja wa mazoezi ili kumshawishi kocha Fadlu.

"Kama binadamu ni lazima kidogo ujisikie vibaya, lakini kwenye soka ni kawaida, ni lazima upambane ili upate nafasi, umshawishi mwalimu ili kukupa kile ambacho anaona utakileta uwanjani, yaani wala sina hofu na wala mashabiki wasiwe na wasiwasi nitacheza tu, na ikumbukwe wote tunaipambania timu moja," alisema.

Wakati Chasambi akisema hayo, tayari klabu hiyo imemsajili winga mwingine, Elie Mpanzu ambaye ataanza kuitumikia timu hiyo katikati ya Desemba mwaka huu.

Usajili wa mchezaji huyo utazidi kuleta ugumu wa namba kwenye kikosi hicho, kwani Mpanzu mbali na kuwa mzoefu wa michezo ya kimataifa, lakini pia ni mmoja wa mawinga wenye uwezo wa kufunga mabao kama mshambuliaji.