Camara, Diarra wachuana kwa 'clean 'sheets'

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:37 AM Oct 09 2024
Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga
Picha:Mtandao
Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga

MALIGOKIPA wawili kutoka Afrika Magharibi, Moussa Camara wa Simba na Djigui Diarra wa Yanga, ni moja kati ya makipa wanne wanaoongoza kwa kusimama langoni mechi nyingi bila kuruhusu wavu wao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.

Camara, raia wa Guinea na Diarra kutoka nchini Mali, wamefikisha 'clean sheets' nne mpaka sasa katika michezo ya Ligi Kuu ambayo imeingia kwenye raundi ya saba.

Camara amepata 'clean sheets' zake aliposimama langoni kwenye michezo ambayo timu yake ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, mabao 4-0 dhidi ya Fountain Gate, mabao 2-0 dhidi ya Azam FC na bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Kwa upande wa Diarra, mechi alizopatia 'clean sheets' ni ile ambayo Yanga ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar, bao 1-0 dhidi ya KenGold, bao 1-0 dhidi ya KMC na mabao 4-0 dhidi ya Pamba Jiji.

Hata hivyo, Camara amesimama langoni mechi tano, moja akishindwa kulinda 'clean sheets', aliporuhusu mabao mawili, Simba ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, huku Diarra akidaka mechi nne na zote amefanikiwa kutoruhusu wavu wake uguswe.

Makipa wengine wenye 'clean sheets' nne ambao ni Watanzania ni, Patrick Munthali wa Mashujaa FC na Mussa Mbisa wa Prisons.

Tofauti ni kwamba makipa hawa wakaa langoni mara sita, hivyo wameruhusu wavu wao kuguswa katika michezo miwili ya Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa Kitengo cha Takwimu cha Dawati la Michezo Nipashe, makipa wenye 'clean sheets' tatu mpaka sasa ni Mohamed Mustafa na Zuberi Foba, wote wa Azam FC, Allan Ngeleka wa Dodoma Jiji, Denis Donis wa JKT Tanzania, Metacha Mnata wa Singida Black Stars, Yona Amosi wa Pamba Jiji na Fabien Mutombora wa KMC.