CHADEMA yaweka nguvu uchaguzi Serikali za Mitaa

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:25 AM Oct 09 2024
Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.

IKIWA zimebaki siku mbili kuanza kwa uandikishwaji wa wananchi Daftari la Wakazi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, alisema ni muhimu kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari hilo Oktoba 11 hadi 20 ili waitumie vizuri haki yao ya kuchagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Alisema CHADEMA kimeamua kuongeza kasi ya uhamasishaji kwa sababu wameona suala hilo halijapewa uzito mkubwa wakati siku za kujiandikisha zinakaribia.

“Nimewaita kupitia kwenu kuwatangazia Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura ambao ni wakazi wa mtaa wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, kuanzia Oktoba 11 mpaka 20, kote nchini wanapaswa mjitokeze kwenda kujiandikisha kwa wingi,” alisisitiza.

Alisema wamefanya tathmini na kuona kuwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), haifanyi jitihada za kutosha za kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Wakazi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa zikiwa zimebaki siku mbili za uandikishaji kuanza.

Aidha, alisema hata halmashauri za wilaya zilizopewa jukumu la kusimamia uandikishaji huo kwa mujibu wa mwongozo na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hazijafanya jitihada za kutosha kuelimisha jamii kuwa zina wajibu wa kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura.

Mnyika alisema kutokuwa na elimu kunajaza imani kwa wananchi kuwa wanaweza kupiga kura kwa kutumia kadi za mpigakura walizonazo jambo ambalo sio la kweli.

“Niwaambie Watanzania wote wafahamu kuwa na kadi ya mpigakura, kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura lililo chini ya Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC) hakutoi uhalali wa mwananchi kupiga kura kwenye uchaguzi wa vijiji na vitongoji kama jina lako halijaingia kwenye orodha ya wapigakura inayoandikwa hivi sasa,” alisema.

Alitoa rai kwa viongozi wa dini, asasi, taasisi za kiraia na vyombo vya habari kutumia wajibu wao kuhamasisha wananchi kwenda kujiandikisha, ili wapate haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi kwenye uchaguzi huo.

Alisema wanachama wa chama hicho kwa sasa wametawanyika sehemu mbalimbali wakihamasisha umma kujiandikisha, lakini jitihada za chama hicho peke yake hazitoshi kwa kuwa na wao pia wanajiandaa kwa kuweka wagombea katika uchaguzi huo.

Alitoa rai kwa wanachama wa chama hicho ha hata wasio wanachama wanaopenda demokrasia, ukweli na uadilifu kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali kupitia chama hicho kwa kuwa uchaguzi huo ni mkubwa na unahitaji wagombea wengi.

Mnyika alisema chama hicho pia kitaweka mawakala katika vituo vinavyoandikisha wapigakura ili kuhakikisha kuwa wapiga kura wasio halali hawaingizwi katika madaftari hayo na kutoa wito kwa yeyote anayetaka kushiriki kwenye uwakala ajitokeze na kuwasiliana na chama katika ngazi yoyote.

“Tukifanikiwa kulinda haki, ukweli, uhuru, demokrasia, maendeleo kupitia uandikishaji wa wapigakura safari itakuwa rahisi sana kwenye hatua nyingine zinazofuata.” Alisema.

Aidha, alitoa rai kwa Watanzania wote kutoa msaada wa hali na mali kama vile maji ya kunywa kwa mawakala wa chama hicho watakaojitolea kusimamia uandikishaji huo kwa siku kumi ili haki itendeke.