Lissu akutana na wakili wake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:36 AM Oct 09 2024
Lissu akutana na wakili wake
Picha: Mtandao
Lissu akutana na wakili wake

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amekutana na kufanya mazungumzo na mwanasheria wake, Bob Amsterdam.

Septemba 25, mwaka huu, Lissu alisema amezungumza na Amsterdam kuhusu kusudio la kufungua kesi dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya simu ambayo inadaiwa kuvujisha mawasiliano yake ya simu, hata kufanikisha shambulio la kupigwa risasi miaka saba iliyopita.

Alifikia hatua hiyo baada ya gazeti la The Guardian la Uingereza kuripoti kesi inayoendelea mahakamani nchini humo iliyofunguliwa na aliyekuwa Ofisa Usalama wa kampuni hiyo ya mawasiliano dhidi ya kampuni mama kwa kumwachisha kazi kutokana na anachodai kufanya uchunguzi dhidi ya wafanyakazi waliovujisha taarifa hizo.

Katika ukurasa wake wa X jana, Lissu alitupia picha akiwa na Amsterdam akiandika maneno yanayosema, “Mapema leo katika mkutano wa asubuhi na Bob Amsterdam huko Steigenberger Wiltcher’s Brussels.”

Lissu alishambuliwa kwa risasi (inadaiwa risasi 38 zilielekezwa kwake akiwa katika gari lake) Septemba 7, 2017, kwenye eneo la nyumba za viongozi wa serikali jijini Dodoma.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari siku hiyo, Lissu alisema, “Nimewaambia walianzishe, leo (Septemba 25) nimezungumza na Bob Amsterdam, nimemwambia una mamlaka kamili ya kulianzisha. Hatujazungumza madai ya fedha, ninafikiri yatakuwa mengi sana, hatujayajadili bado.”

Alisema tukio hilo katika tafsiri ya sheria, ni kitendo cha ugaidi kwa mujibu wa sheria za Tanzania; amepata ulemavu wa kudumu, hawezi kutembea sawasawa.

Alisema anatembea na risasi mgongoni na mwili umejaa vyuma kwenye goti mpaka kwenye nyonga, makovu ya risasi 16 zilizompata kati ya 38 na ya operesheni 25.

RIPOTI YA THE GUARDIAN

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti The Guardian la Uingereza, aliyekuwa Ofisa Usalama wa kampuni hiyo ya mawasiliano ya simu, amefungua kesi nchini humo akidai kufukuzwa kazi bila haki baada ya kupinga hatua ya kutoa data za simu za mwanasiasa Tundu Lissu mwaka 2017 na kuvujishwa bila ridhaa yake.

Anadai kuwa akiwa mfanyakazi wa kampuni hiyo, alivutiwa na mazungumzo fulani yaliyofanyika kwenye mkutano wa mtandaoni na yeye akiwa mshiriki, na kwamba alishtuka kwamba kuna jambo linaendelea pasipo yeye kushirikishwa kama mkuu wa idara.

Anadai alianzisha uchunguzi binafsi na kubaini kulikuwa na mawasiliano yasiyo ya afya baina ya kampuni na idara fulani ya serikali, ambayo yalifanyika kupitia mtandao wa WhatsApp, kampuni hiyo ya simu ikivujisha taarifa binafsi za simu za Lissu.

"Uvujishaji ulianzia tarehe 22 Agosti 2017, lakini kuanzia Agosti 29, 2017 kukawa na uvujishaji mkubwa wa taarifa za Lissu mbashara (live tracking). Taarifa hizo zilihusu maeneo aliyopo Lissu, simu zinazoingia na kutoka zikisikilizwa na SMS (ujumbe) zake zikisomwa,” alidai.