Mtandao wa X warudi Brazil, Elon Musk akubali yaishe

By Allan Isack , Nipashe
Published at 04:09 PM Oct 09 2024
Mtandao wa X warudi Brazil
Picha: Mtandao
Mtandao wa X warudi Brazil

MTANDAO wa Kijamii wa X zamani ukijulikana Twitter ni rasmi sasa utaanza kutumika tena nchini Brazil, baada ya Mahakama ya Juu nchini humo kuwaondolea zuio la kufunga akaunti za jukwaa hilo.

Mtandao huo,uliondolewa zuio kutokana na uamuzi uliotolewa na Jaji Alexandre de Moraes,alisema Mahakama imeridhia kurudishwa kwa shughuli za X baada ya kulipa faini.

Alisema kulingana na taarifa zilizotolewa na mtandao huo,wamekubali kulipa faini ya Sh.bilioni 13 ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani milioni 5.1.

Kadhalika mtandao wa X umekubali kuteua mwakilishi wa eneo hilo,kama ilivyotakiwa na sheria za nchi ya Brazil.

Awali mtandao huo,ulilalamikiwa na serikali ya nchi hiyo,kwa kueneza habari potofu kuhusu uchaguzi wa Rais wa Brazil mwaka 2022, hivyo kufanya akaunti za watumiaji wake kufungiwa.

Kitendo cha kufungiwa kwa akaunti kilisababisha watumiaji wa jukwaa hilo, kutumia VPN kama njia mbadala ya kufikia huduma huku wakiilalamikia serikali juu ya uvunjwaji wa haki ya kupata taarifa na uhuru wa kujieleza.