Anne Makinda: Ushindi ni hesabu, wanawake nendeni mkajiandikishe

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 03:31 PM Oct 09 2024

SPIKA mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda.
Picha: Thobias Mwanakatwe
SPIKA mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda.

SPIKA mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Anne Makinda,amewataka wanawake katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wajiandikishe,wagombee nafasi za uongozi na kwenda kupiga wasipofanya hivyo itakuwa imekula kwao kwani ushindi ni hesabu.

Makinda ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa, akizungumza leo kwenye kongamano la wanawake na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 linalofanyika mjini Singida na kuwashirikisha wanawake wote wa Mkoa wa Singida, amesema wanawake wanatakiwa kufanya maajabu katika chaguzi hizo kwa kuhakikisha rais anakuwa mwanamke,wenyeviti wa vitongoji,vijiji na mitaa nao wanakuwa wanawake hadi dunia ishangae.

"Tujiandikishe na tukapige kura tusipopiga kura imekula kwetu kwani ushindi ni hesabu,maana mama (rais) anasifika sana mara asante kwa maji,asante kwa barabara basi nyie mnafikiri mama anapita asubuhi,hapana ni hesabu hata viongozi wetu wa mitaa,vitongoni ni hesabu," amesema.

Naye Mkuu wa  Mkoa wa Singida,Halima Dendego, amesema wanawake kwa kutambua kuwa wao ndio nguzo ya uchumi wahakikishe wanasimamia malezi ya watoto wao wasiache walelewe n mitandao ya kijamii.