Ushetu watumia tamasha kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mitaa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:05 PM Oct 09 2024
Ushetu watumia tamasha kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mitaa
Picha: Shaban Njia
Ushetu watumia tamasha kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi mitaa

MKUU wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita amewasihi wananachi wa Halmashauri ya Ushetu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kupata nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka ifikapo Novemba 27 mwaka huu.

Mhita aliyabainisha hayo jana wakati akitoa elimu ya mpiga kura katika tamasha la uhamasishaji lililofanyika katika kata ya Nyamilangano-Ushetu, alisema, kila kila mwananchi anaumuhimu wa kushiriki uchaguzi kwani ndio njia sahihi ya kuchagua wawakilishi wahihi watakao wasemea changamoto zao.
 
Amesema, ili upate nafasi ya kushiriki uchaguzi huo lazima uwe umejiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambalo zoezi hilo litaanza Oktoba 11 mpaka 20 mwaka huu na wale wenye umri wa kupiga kura watapata nafasi ya kujiandikisha hivyo kila mmoja anawajibu wa kuchagua na kuchaguliwa pale atakapopata nafasi ya kushiriki.
 
“Tujitokeze kwa wingi tukajiandikishe ili yale yote ambayo tumekuwa tukilalamika yapate ufumbuzi, nan jia ya kufikisha hizo salamu inaanzia kwenye ngazi ya kitongoji, mara nyingi mtu unaweza usione umuhimu wa Mwenyekiti wa kitongoji, kijiji au mtaa na ukakimbilia kwa Diwani lakini kama huna mwenyekiji wa kijiji sawa kazi bure” amesema Mhita.
 
Ameongeza”Wakati mwingine sio kilo lazima ifike kwa diwani au Mbunge wa jimbo, zipo nyingine zinaishia ngazi hizi za chini yaani kitongoji, kijiji na mitaa na ili nafasi hizo zipatikane lazima mjitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura na kuchaguzi viongozi hao nasio vinginevyo”.
 

Aidha amewasihi wananchi wenye uwezo wa kuongoza kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo kwani viongozi bora wanatoka kwa wananchi wenyewe na kila mwananchi anahaki ya kuchagua na kuchaguliwa.
 
Tamasha hilo liliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu kama sehemu ya kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la uandikishaji kwenye daftari la kudumu wa wapiga kura lenye kauli mbio isemayo ”Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi jitokezeni kushiriki uchaguzi”.

2