Lukuvi aahidi Uchaguzi kuwa huru na haki

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 06:52 PM Oct 09 2024
Lukuvi aahidi Uchaguzi kuwa huru na haki.
Picha: Mpigapicha Wetu
Lukuvi aahidi Uchaguzi kuwa huru na haki.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Willium Lukuvi amevihakikishia vyama vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki na hakutakuwa na ubadhirifu wa aina yoyote katika kutangaza washindi.

Hayo ameyasema jana Oktoba 8 Jijini Dar es Salaam katika siku ya pili wa  mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitakavyoshiriki uchaguzi. 

Lukuvi alisema  Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza awaambie viongozi hao watoè wasiwasi kwani uchaguzi wa  2024/25 utatenda haki kwa asilimia zote hakuna atakayedhulumiwa haki na Serikali imejipanga kwakila atakepata kura nyingi ndiye atakayetangazwa kuwa mshindi. 

“Nawahakikishieni uchaguzi wa mwaka huu utaenda vizuri kwa kufuata sheria na kanuni zilizowekwa, katika kila ushindani lazima kuwepo na mshindi bila kujua atatoka chama gani hivyo atakayekuwa na kura nyingi atatangazwa bila kuangalia chama” alisema 

Wakati huohuo viongozi wakuu wa vyama hivyo wamempongeza na kumsifia Waziri Lukuvi kwa kufurahishwa na mwenendo wake wa kutembelea vyama hivyo kitendo ambacho wamedai hakijawahi kutokea. 

Makamu Mwenyekiti NCCR Mageuzi, Joseph Selasini aliòmba baadhi ya kanuni kutenguliwa kwani zinaleta ugumu katika mchakato mzima wa uchaguzi kwa vyama ambavyo ni vichanga kutomudu kutokana na hali ya kifedha ya vyama akitolea mfano sheria ya ugongaji wa mihuri kwa wagombea. 

"Tunaomba uchaguzi huu usiwe kama uchaguzi uliopita ili kuepusha machafuko, na sisi tunaahidi uchaguzi huu utakuwa wa amani kwani tumeridhishwa na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R ambayo ndani yake kuna maridhiano” alisema 

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF) Prof.Ibrahim Lipumba amesema kumekuwa na kukinzana kwa kanuni na miongozo katika baadhi ya kanuni zilizowekwa za kuongoza chaguzi hivyo kuomba kanuni hizo ziangaliwe upya ili kuleta afueni kwa baadhi ya vyama vichanga. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama cha NLD, Doyo Hassan amesema kwa kufuatia hatua ya Waziri  kutenga muda wake na kutembelea vyama vya siasa inaonyesha dhahiri dhamira ya Rais Samia kuviunganisha vyama na Serikali na kudumisha na tayari kuanza kwa falsafa yake ya 4R. 

“Haya ni mabadiliko makubwa sana ndani ya sekta ya siasa Rais anatupa moyo hivyo nasi tunaahidi tuko pamoja nae na tunaahidi uchaguzi utakuwa wa utulivu bila magomvi yoyote” amesema Doyo

 Katika siku ya pili ya ziara hiyo  Waziri Lukuvi alitembelea vyama vinne vikiwemo UDP, CCKCUF na NLD. 

Tayari ameshatembelea chama cha  UPDP, ACT Wazalendo, UPDP na CCK katika siku ya kwanza ya ziara hiyo.