Balozi Nchimbi amjibu Mnyika

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 08:54 PM Oct 09 2024
Balozi Nchimbi amjibu Mnyika
Picha: Mtandao
Balozi Nchimbi amjibu Mnyika

CHAMA Cha Mapinduzi CCM kimejibu kauli iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika aliyoilaumu TAMISEMI na CCM kwamba hawafanyi jitihada za kutosha kuhamasisha watu kujitokeza kujiandikisha kwenye dafatari la wakazi katika uchaguzi wa serikali za mtaa.

Mnyika aliongeza hata Halmashauri zilizopewa jukumu la kusimamia uandikishaji huo kwa muujibu wa mwongozo na kanuni za Serikali ya Mitaa hazijafanya hivyo.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi akiwa ziarani Malampaka Maswa mkoani Simiyu  amesema ameona katika mitandao ya kijamii kiongozi mmoja wa upinzani bila kimtaja jina analalamika kuhusu suala hilo.

"Kiongozi huyo amesema CCM na TAMISEMI kwa makusudi hawahamasishi watu kujiandikisha, hawahamasishi watu kupiga kura nikacheka nikasema hawa wenzetu hawa. Sisi mikoa yote 18 tunazunguka tunahamasisha si mnatusikia huko kwenye redio.

"Tunahamasisha watu wajiandikishe, watu wapige kura wanaCCM na wasio wanaCCM kwa sababu tunajua hata wasiokuwa wanaCCM wanaipigia kura CCM kwa sababu ya kazi nzuri ambayo chama chetu imefanya" amesema Nchimbi 

Amesema kupitia kauli hiyo alisikilza na kutafakari na kwamba anadhani tayari chama hicho kimeshajua hali ni mbaya kwamba hawatopata kitu katika uchaguzi huu kwa hiyo wanaanza kutafuta kisingizio mapema.

"kama wanavyofanya zile timu kubwa...oooh walitangulia wakaruka ukuta kwani ukuta ndiyo unaocheza? Watu ndiyo wanaocheza visingizio waache twendeni tukatafute kura, wao waombe na sisi tuombe visingizio hivi ni vya kitoto" amesema Nchimbi huku akishangiliwa.