HASSAN NASRULLAH: Kiongozi aliyeongoza mapambano kutetea wanyonge hadi shujaa muhimu vitani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:24 PM Oct 09 2024
Sayyed Hassan Nasrallah, enzi za uhai wake.
PICHA: MTANDAO
Sayyed Hassan Nasrallah, enzi za uhai wake.

SAYYID (baba) Hassan Nasrullah, aliyejulikana kama Sayyid wa viongozi wa ulimwengu wa Kiarabu, alipewa jina la Sayyid wa muqawama (mapambano) na ukombozi.

Ni kwa sababu ya msisitizo wake hasa  kwenye kanuni na maadili katika kuwatetea wanaodhulumiwa, pamoja na  mapambano yake makali dhidi ya ubeberu. 

Mtaalamu wa Ushauri wa Kitamaduni wa Ubalozi wa Iran nchini Tanzania Maulid Sengi, anamzungumzia  shahidi Nasrullah,  akisema alizaliwa Agosti 31, 1960 katika Kijiji cha Al Bazourieh Kusini mwa Lebanon. 

Mwaka 1976  akiwa kijana, alikwenda Najaf, Iraq, kuanza masomo katika seminari na kurejea Lebanon 1978, akiendelea na masomo katika Shule ya Imam al-Muntazar (a.s.).

Ilianzishwa na Sayyid Abbas Mousawi, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah, na wakati huo huo, alijishughulisha na siasa katika eneo la Bekaa.  

Baada ya kuasisiwa Hizbullah, Nasrullah alishika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uanachama katika Baraza la Uongozi la Hizbullah, lakini hakujiweka mbali, akiendelea kutafuta elimu hadi alipokwenda Qum nchini Iran,  1989  kukamilisha masomo yake.  

Sengi anasema mashambulizi makubwa ya Israel dhidi ya Lebanon na mapambano ya Hizbullah dhidi ya utawala huo hayakumruhusu kukaa Qum kwa zaidi ya mwaka mmoja, alirejea Lebanon kwa mara nyingine na kujiunga na wenzake katika kukabiliana nayo. 

Mwaka 1992, Abbas Mousavi, Katibu Mkuu wa Hizbullah wakati huo na mwalimu wa Nasrullah aliuawa.

 "Kupanda ngazi kwa Nasrullah katika harakati hiyo, kuliiondoa Hizbullah katika mzingo wa ulinzi na usalama na kufungua medani mpya ya uwepo wa Hizbullah katika muundo wa kisiasa wa Lebanon.

 "Mwaka wa 2000, wakati wa mazungumzo kati ya Yasser Arafat na maofisa wa Marekani na Israel ili kutatua mzozo katika eneo la Asia Magharibi yaliyokwama. Jeshi la Israel lilijiondoa katika maeneo yaliyokuwa yakikaliwa kwa mabavu ya kusini mwa Lebanon katika hatua ya upande mmoja na bila ya kupata lolote kutoka Hizbullah. 

 "Majeshi la Israel yaliondoka katika maeneo yote yaliyokaliwa kwa mabavu, isipokuwa mpakani na mashamba ya Shabaa.”

 Sengi anasema kushindwa huko mbali na kuimarisha msimamo wa Hizbullah kama harakati ya mapambano, kulimfanya Nasrullah apate mafanikio makubwa kati ya Waarabu na Waislamu kwa ujumla.

“Kuanzia hapo akatambuliwa kama mtu muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu," anasema Sengi.

 Anasema kwa upande mwingine, kwa kuegemea kwenye mafanikio hayo, Hizbullah ya Lebanon iliimarisha uwepo wake katika uga wa kisiasa kwa kadiri kwamba, mbali na kushinda viti vingi vya bunge, pia ilishika usukani wa idadi ya wizara za serikali ya nchi hiyo.

 Juhudi zisizokoma za Hassan Nasrullah katika kutetea haki za wanyonge na kubeba bendera ya Kambi ya muqawama kwa miaka mingi, ziliandamana na mafanikio na ushindi wa wapiganaji .

Jambo hilo lililomfanya  Nasrullah daima kuwa miongoni mwa walengwa wakuu wa idara za ujasusi na  utawala wa Israel.

 Anasema baada ya miaka mingi ya misimamo ya kishujaa na juhudi kubwa za kuendeleza kambi ya mapambano na muqawama, jioni ya Ijumaa Septemba 27, 2024 Hassan Nasrullah, aliuawa.

“Alifanikiwa kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi  katika jinai ya utawala wa Israel na mashambulizi yake dhidi ya makazi ya raia eneo la Dhahiya, kusini mwa Beirut.”

 Nasrullah alikuwa ni Katibu Mkuu wa tatu wa Hizbullah, chama cha kisiasa na kijeshi cha Lebanon kilichoasisiwa mwaka 1982. 

 Chini ya uongozi wake, Hizbullah iliimarika na kuwa na nguvu muhimu ya kikanda iliyofanikiwa kuilazimisha Israel kuondoka Kusini mwa Lebanon mwaka 2000, baada ya operesheni za kijeshi zilizojumuisha kuwarudisha huru wafungwa wa Kilebanoni. 

 Hassan Nasrullah aliuawa kwa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na vikosi vya Israel

na kuongezeka kwa tofauti kati ya Hizbullah na harakati za kikundi cha Amal, hali iliyosababisha Baraza la Uongozi kumtaka arudi nyumbani.

 Mwaka 1978, Hassan Nasrullah akiwa na umri wa miaka 18, alifunga ndoa na Fatimah Yassin. Akijaliwa kupata watoto watatu wa kiume ambao ni Muhammad Hadi, Muhammad Jawad na Muhammad Ali, pamoja na binti anayeitwa Zaynab.

 Muhammad Hadi, mtoto  mkubwa, aliuawa Septemba 12, 1997 Miladia, katika mapambano dhidi ya vikosi vya ulinzi vya Israel Kusini mwa Lebanon. 

 Mwili wake ulibakia  mikononi mwa Israel na  baada ya mwaka mmoja, ulirejeshwa  Lebanon kupitia operesheni ya kubadilishana wafungwa kati ya Israel na Hizbullah.

 Shughuli za kijamii na kisiasa za Hassan Nasrallah zilianza tangu akiwa mdogo.

 Baada ya kumaliza sekondari mwaka 1975 Miladia, aliteuliwa kuwa kiongozi wa kikundi cha harakati za Amal katika kijiji chake cha al-Bazuriyya.

 Baada ya kurejea kutoka Najaf mwaka 1979, alijiunga na ofisi ya kisiasa ya harakati za Amal na kuwa mwakilishi wa harakati hizo katika bonde la Biqaa. 

 Mwaka 1982, akiwa pamoja na kundi la wanazuoni na wanafunzi wa kidini waliohamasishwa na mapambano, alijitenga na kundi la harakati za Amal na kuanzisha kundi la Hizbullah ya Lebanon.

 Kuanzia mwaka 1982 hadi 1992 Nasrullah alitumia muda wake wote Hizbullah na kwamba mbali na kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah, pia alishiriki  kuandaa vikosi vya upinzani na kuanzisha vikundi mbalimbali vya kijeshi. 

 Alikuwa Naibu wa Ibrahim Amin al-Sayyid, kiongozi wa Hizbullah mjini Beirut, na kwa kipindi fulani alikuwa ni Naibu Mtendaji wa Hizbullah ya Lebanon. 

 Sengi anasema Hassan Nasrallah alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kwa makubaliano ya wanachama baada ya kuuawa kwa Abbas Mousawi, Februari 16, 1992, akichukua jukumu hilo akiwa na miaka 32.

 Kwa kuangalia mchango wake binafsi pamoja na jitihada za Hizbullah kukomboa Kusini mwa Lebanon mwaka 2000, baada ya miaka 22 ya uvamizi wa Israel, pamoja na ushindi katika vita vya siku 33, Hassan Nasrullah, alipatiwa jina la "Sayyid wa upinzani  au baba wa upinzani".