KUELEKEA KUMBUKIZI YA NYERERE: Ahadi 10 za mwana TANU ni muhimu zaidi sasa

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 08:20 PM Oct 09 2024
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere
Picha: Mtandao
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere

JUMATATU ijayo Oktoba 14, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, anatimiza miaka 25 tangu kufariki dunia, licha ya kutwaliwa, ameacha hazina ya tunu ambazo haziwezi kuchakaa au kumaliza muda wa matumizi.

Ndiye aliyeasisi ahadi 10 za mwanachama baada ya uhuru ili kusimamia maadili na utumishi wa umma.

TANU inajiwekea ahadi hizo zilizopewa jina la 'Ahadi za Mwanachama', ili zisimamie kikamilifu kwa ajili ya kuimarisha chama na ustawi wa taifa kwa ujumla.
 
 Tukijikumbusha ahadi ya kwanza anasema, binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja, ya pili ni utumishi; nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, huku ya tatu ikiahidi kujitolea nafsi na nguvu kuondoa umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma".
 
 Vilevile kuna ahadi ya nne inakataa ufisadi; "rushwa ni adui wa haki. Sitapokea wala kutoa rushwa. Ya tano ni 'cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu wala cha mwingine kwa faida yangu".
 
 Lakini ipo ya kutafuta elimu ni ahadi ya sita, ikisema; "nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya wote, ya saba inasema;
 Nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu".
 
 Ya nane inasema; "nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko, wakati ahadi ya tisa inakumbusha  kuwa ‘nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU na raia mwema wa Tanganyika na Afrika".
 
 Pamoja na hizo, ahadi ya mwisho ambayo ni ya 10, inasema; "nitakuwa mtiifu na mwaminifu kwa Rais wa Serikali ya Tanganyika".
 
 Nchi inapokaribia kilele cha kumbukumbu ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa, Nipashe inazungumza na baadhi ya wadau wa siasa ili kupata maoni yao kuhusu ahadi hizo na kama zina nafasi bado na iwapo zinahitaji kuendelezwa.
 
 ZIWE KWENYE KATIBA
 
 Ni msimamo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha  Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, anasema ili ahadi hizo zifanye kazi, ni vyema mchakato wa katiba ufanyike na kuziingiza huko ili zisimamiwe vizuri.
 
 "Ahadi nyingi kati ya hizo 10, hazigusi siasa, hivyo ni vyema zikaondolewa kwenye chama na kuingizwa kwenye katiba mpya ili zipewe uzito mkubwa na unaostahili," anasema Dk. Anna.
 
 Anafafanua kuwa licha ya kuwapo kwa ahadi hizo, ambazo zinatakiwa kusimamiwa na wanachama wenyewe, bado mambo yanakwenda kinyume na jinsi yanavyotakiwa kutekelezwa.
 
 "Kwa mfano ripoti nyingi za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kuwapo kwa rushwa na ufisadi katika taasisi mbalimbali pamoja na za umma, kitendo kinachoonyesha kuwa ahadi ya nne haizingatiwi," anasema.
 
 Anasema kile ambacho Mwalimu Nyerere alikuwa akikipigania kupitia ahadi hizo inaelekea kimekwama kutokana na kuwapo vitendo ambavyo vinavyofanywa na baadhi ya wanachama kinyume na inavyotakiwa.
 
 "Vilevile, kuna ahadi ya umoja, nitashirikiana na wenzangu wote kuijenga nchi yetu, cha ajabu tunashuhudia jinsi ambavyo wanasiasa wanabaguana hadharani, wakisema sehemu ambayo wapigakura wamechangua upinzani, serikali haiwezi kuleta maendeleo, inakuwaje," anahoji?
 Anaeleza kuwa, kauli ya aina hiyo ni kinyume na ahadi za mwanachama hasa ya saba inayohimiza ushirikiano kwa ajili ya ujenzi wa taifa, na kuongeza kuwa sehemu ya ahadi hizo haifanyiwi kazi.
 
 “Kwa maoni yangu, CCM iachiwe sehemu ya ahadi ya tisa inayosema; nitakuwa mwanachama mwaminifu wa TANU/CCM  lakini upande wa kuwa raia mwema wa Tanzania na Afrika uingizwe katika katiba," anasema.
        
    ZIMEONDOKA NA MWALIMU 
 Kada wa CHADEMA, Suzan Lyimo, anasema, ahadi hizo zilitekelezwa enzi za Nyerere lakini ameondoka nazo baada ya kufariki dunia.

 Anafafanua kuwa hazitelekezwi kama ilivyokusudiwa na zimepuuzwa.
 
 Anatoa mfano ahadi ya nane; "nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko", kwamba siku hizi anayesema ukweli hatakiwi, anaonekana ni adui ndani na hata nje ya chama.
 
 "Ukweli ni kwamba Nyerere ameondoka na ahadi za mwanachama, kwani kuna mengi yanaendelea kufanywa kinyume na malengo ya ahadi hizo 10 kana kwamba hazipo," anaeleza Suzan.
 
 Mbunge huyo wa zamani wa CHADEMA, anataja rushwa, akisema zamani ni adui namba moja wa haki na maendeleo. Kwa sasa imekuwa si adui wa haki  wala mkwamishaji maendeleo pengine ni rafiki wa watu. Kwa kuwa wengi wanatoa na kupokea kama  jambo la kawaida badala ya kuikimbia.

Imepewa majina mengi ikiwamo takrima.
 
 "Tuambiane ukweli bila kificho kuwa, ahadi 10 za mwanachama ni kama hazipo tena, kwani tukianza kutaja mambo yanayotendeka kinyume na ahadi hizo ndani ya nchi ni mengi," anasema.
 
 Anasema ahadi hizo zinapinga ubaguzi, wa rangi, kabila, dini na aina myingine za kubaguana na kuhimiza umoja na mshikamano, lakini badala yake Watanzania sasa wanabaguana kwa itikadi za vyama vya siasa.
 
 Mwaka huu kuna mwanachama wa CCM alitamka hadharani kuwa wanapowapoteza watu, polisi wasihangaike kuwatafuta watu hao, kitendo kinachokwenda kinyume na ahadi zao wenyewe, anasema.
 
 Anasema ahadi zote 10 zilikuwa na lengo zuri, na kwamba zimekwama kufanya kazi kwa kukosa usimamizi na kusababisha wachache wanaojaribu kuzisimamia, kuonekana kama maadui.