'Macho ya watoto yapo hatarini'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:25 PM Oct 09 2024
'Macho ya watoto yapo hatarini'
Picha:Mpigapicha Wetu
'Macho ya watoto yapo hatarini'

JAMII imetakiwa kuwalinda afya ya macho ya watoto kwa kuwaepusha na vitu vinavyohatarisha macho yao ikiwa kuzingatia muda wanaotumia kwenye runinga, simu pamoja na kompyuta.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Dk. Hamad Nyembea ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua maadhimisho ya Wiki ya Macho duniani yaliyofanyika katika kituo cha Afya Makole jijini Dodoma yenye kauli mbiu ‘Penda macho yako, mhamasishe mtoto kupenda macho yake’. 

Amesema zaidi ya watu milioni 1.6 wamehudumiwa kwenye kliniki za kutoa huduma za macho kwa mwaka 2023, kati ya hao asilimia 42 waliopata huduma walikuwa na umri chini ya miaka 15 huku  asilimia sita ya watoto hao wakiwa  wenye ulemavu wa kutokuona. 

Dk. Nyembea amesema miongoni mwa vyanzo vikubwa vya matatizo ya macho kwa watoto na vijana ni mzio, upeo mdogo wa macho kuona unaorekebishika kwa miwani na majeraha kwenye macho.