Bashungwa ataka utafiti wa bidhaa sokoni

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 08:35 PM Oct 09 2024
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.

WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema Ili kuepuka kufanya biashara moja katika soko moja hali inayosababisha baadhi ya wafanyabiashara kukosa soko ni vema ukafanyika kutafiti kabla ya kuingiza bidhaa sokoni.

Bashungwa amesema maafisa masoko na biashara wanatakiwa kufanya utafifi wa bidhaa na kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili biashara zao ziwe endelevu.

Ameyasema hayo wakati akizindua Soko la Bwilingu Mjini Chalinze ambapo amesema kukiwa na utafifi wa masoko itasaidia kuibua mitaji ya wafanyabiashara hao na kuondoa malalamiko ya kutouza bidhaa zao.

Amepongeza utaratibu wa Halmashauri ya Chalinze kuwa na miradi ya kimkakati kupitia mapato ya ndani ambayo pia inatumika kuongeza vyanzo vya mapato ikiwemo soko hilo ambalo limejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 1.7 .

Katika hatua nyingine Bashungwa amewataka wazazi na walezi kuwapa haki ya elimu watoto wao kwani Serikali imeondoa vikwazo vya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwa kujenga shule katika maeneo mbalimbali.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, baadhi ya wazazi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jakaya Kikwete ambapo amesema shule zimeendelea kujengwa kwenye kila kata hapa nchini na maeneo yanayobainika shule kuwa mbali tatizo hilo linatafuliwa kwa kujenga shule nyingine.

Akiwa Chalinze Bashungwa ameweka jiwe la Msingi katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Jakaya Kikwete, nyumba za wakuu wa idara, na kuzindua Soko la Bwilingu.