Munisi apewa 'kongole' kongamano la uchaguzi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:01 PM Oct 09 2024
Munisi apewa 'kongole' kongamano la uchaguzi
Picha:Mpigapicha Wetu
Munisi apewa 'kongole' kongamano la uchaguzi

DIWANI wa Kata ya Machame Magharibi iliyopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Martin Munisi, ameanzisha kampeni maalum ya kuombea amani na utulivu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu nchini kote.

Aidha, amewasihi vijana na wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi, ili kujenga usawa katika ngazi za maamuzi, huku pia akitumia kongamano hilo kuonya vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake.

Leo Oktoba 9, 2024, Munisi, aliwaongoza wakazi wa kata hiyo, kwa nyakati tofauti akiwa vijiji vya Kyeer na Nronga, kuombea uchaguzi huo ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Kabla ya kongamano hilo la maombi yaliyowahusisha viongozi wa dini,  Diwani Martin Munisi, aliwataka wananchi wote kujitokeza kujiandikisha kwenye taftari la mtaa, kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu katika Wilaya hiyo.

Katika kongamano hilo la kuombea uchaguzi, Diwani Munisi, ameeleza wazi kuwa hakuna mtu ambaye siasa haimhusu, akisisutiza  siasa inawahusu wananchi wote na siasa ndiyo inayoamua ulale saa ngapi na uamke saa ngapi.

"Ndugu zangu, siasa ndiyo inayoamua juu ya elimu yetu, siasa ndiyo inayoamua juu ya afya, siasa ndiyo inayoamua namna ya wewe kuabudu kwa utaratibu gani.

... Ukihitaji kitambulisho cha mkazi, bado mwanasiasa atatakiwa kukuandikia barua ya utambulisho. Hakuna mtu ambaye siasa haimhusu."

Muda mfupi, baada ya maombi, wasimamizi wa uchaguzi katika Kata hiyo, Rosemary Mmary na Taufick Shoo, kwa nyakati tofauti, walipata fursa ya kutangaza ratiba ya uchaguzi huo na kutoa elimu kwa wananchi wa Machame Magharibi.

Anandumi Kimaro, Mkazi wa Kijiji cha Kyeer, alieleza kufurahishwa kwake na utaratibu huo uliofanywa na Diwani wao, wa kuandaa kongamano hilo la kuombea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, huku akisema kuwa wananchi wa kata hiyo watashiriki kikamilifu.

Katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka 2019, ni wanawake 4,171 tu, ndiyo walioshinda nafasi za wenyeviti wa vitongoji, sawa na asilimia 6.7

Huku, wanawake waliochaguliwa kuwa wenyeviti wa mitaa, walikuwa ni 528 kwa nchi nzima, sawa na asilimia 12.6; na wenyeviti wa vijiji, wanawake ni 246 tu, sawa na asilimia 2.1.