RC Dendego: Wanawake gombeeni nafasi za uongozi ili mshiriki katika maamuzi

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 09:11 PM Oct 09 2024


MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego
Picha:Thobias Mwanakatwe
MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewahimiza wanawake mkoani hapa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na uchaguzi mkuu wa mwakani 2025 ili waweze kuwa na nafasi ya kushiriki katika ngazi za maamuzi.

Amesema hayo leo Oktoba 9,2024 wakati akifungua kongamano la wanawake na uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 ambalo linawashirikisha wanawake kutoka wilaya zote za mkoa huu lengo likiwa ni kuwahamasisha kujitokeza kushiriki uchaguzi mwaka huu na mwakani.

Amesema Mkoa wa Singida kwa mujibu wa Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022 unakadiriwa kuwa na jumla ya Watu 2,008,058, kati ya hao wanawake ni 1,012,355 sawa na asilikia 51 na wanaume ni 995,703 sawa na asilimia 49. 

Amesema pamoja na mkoa kuwa na idadi kubwa ya wanawake lakini wenyeviti wanawake ni 96 tu, mitaa ipo 53 wenyeviti Wanawake wapo 03 tu na jumla ya Wanawake katika nafasi ya ujumbe wa Serikali katika ngazi zote wapo 3,125. Aidha, katika nafasi ya Udiwani kati ya Kata 136 za Mkoa, Madiwani Wanawake wapo 04 tu wa kuchaguliwa.

"Takwimu hizi haziridhishi, niwaombe wanawake wenzangu kwa kuanza na uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa twendeni tukapindue meza, tujitokeze kwa wingi kugombea nafasi zote kwani Sifa tunazo, uwezo tunao, vipawa na maarifa ya uongozi tunayo, wanawake ni Jeshi kubwa tukiamua tunaweza," amesema Dendego.