Majaliwa kuzindua Wiki ya Vijana Oktoba 11 Mwanza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:43 PM Oct 09 2024
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa kesho kutwa Oktoba 11, 2024 yanayofanyika mkoani Mwanza ambapo vijana 1,000 watashiriki.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Furahisha na kutaja shughuli nne zinazofanyika kwenye wiki hiyo kuwa ni pamoja na kongamano la fursa na kuwajengea uelewa wa masuala mbalimbali vijana.

Amesema katika kongamano hilo vijana watapata uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024.

Pia, amesema kutakuwa na maandamano ya amani ya vijana na watashiriki 1000 wakiwa wamebeba jumbe mbalimbali ambazo serikali itazifanyia kazi.

“Kutakuwa na Maonesho ambayo hutoa fursa kwa vijana kuonesha bunifu zao na kwa wadau wa maendeleo ya vijana kutoa huduma, elimu na taarifa kwa jamii hususan zile zinazoendana na malengo ya Taasisi zao na zenye lengo la kuleta mabadiliko chanya na kuhamasisha ustawi na maendeleo ya vijana nchini,”amesema.

Amefafanua malengo ya wiki hiyo kuwa ni kuwakutanisha vijana kujadili furs ana changamoto zinazowakabili, kuhamasisha kushiriki katika program mbalimbali za usaidizi wa jamii kwa njia ya kujitolea, kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa namna ya utekelezaji wa masuala ya kiuchumi na kijamii.

“Pia wiki hii inalenga kuwahamasisha vijana watambue kuwa wao ni sehemu ya jamii na wenye jukumu katika kushughulikia changamoto za kijamii kama vile VVU na UKIMWI, Ukiukwaji wa haki za binadamu na watoto, kushiriki katika majukumu ya kiraia ikiwamo kupiga kura na kushiriki vikao vya maendeleo katika jamii,”amesema.

Kuhusu kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, Ridhiwani amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhitimisha sambamba na Kumbukumbu ya Miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere itakayofanyika Kanisa Katoliki la Nyakahoja mkoani Mwanza.

Ametoa wito kwa wananchi na vijana kujitokeza kushiriki katika maadhimisho ya wiki hiyo ya vijana inayofanyika Viwanja vya Furahisha kuanzia Oktoba 8-13, 2024 na Kilele cha Mbio za Mwenge kitakachofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 14, 2024.