Wanufaika mikopo asilimia 10 inaanza

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 12:17 PM Oct 09 2024
Fedha.
Picha: Mtandao
Fedha.

MANISPAA kadhaa zimetoa matangazo kuhusu kurejeshwa tena kwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Hii ni taarifa njema kwa makundi hayo ambayo kwa muda sasa mikopo hiyo ilisimama ili kuandaliwa utaratibu bora.

Ikumbukwe fedha hizo ni zile zinazoleta unafuu kutokana na masharti yake hasa ikilinganishwa na mingine hasa inayotolewa na baadhi ya taasisi binafsi.

Kwa kuwa licha ya kuwa na masharti magumu imetajwa kusababisha baadhi ya wateja  kuwa na hali ngumu, kwa kubambikiwa riba.

Hali ngumu hiyo iwakumbushe wanufaika kadhia inayosababisha mikopo hiyo kuitwa kausha damu’. 

Ni kwa sababu watu wamelazimika kukimbia familia kutokana na riba kubwa walizotozwa na hata wengine kufilisika.

Tangazo la Manispaa ya Ubungo linabainisha kuwa   Sh. bilioni 3.5 zimetengwa kwa ajili ya mkopo huo, na kwamba vikundi ambavyo vinadaiwa fedha za nyuma havitakopeshwa.

 Hili ni angalizo muhimu kwa kuwa wasiorejesha mikopo hiyo nafuu kwa wakati wamechelewesha au kukwamisha mzunguko wa mkopo huo kwenda inavyotakiwa.

Ni kulingana na kanuni zilizowekwa ili kufanikisha kuwainua kimtaji na kimapato wajasiriamani katika makundi hayo.

  Kwa mujibu wa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za mwaka 2019, husasan unaangalizo kwa warejeshaji  mikopo.

Zinabainisha kuwa kikundi kitahesabika kuwa kimepoteza sifa ya kupata mkopo endapo, hakijamaliza kurejesha mkopo uliotolewa awali, au kimetoa taarifa za uongo kwa mamlaka za serikali za mitaa ili  kupata mkopo.

Ikibainika kimetumia fedha za mkopo kwa matumizi tofauti na yale yaliyoombewa bila idhini ya mamlaka ya serikali ya mtaa au kimeshindwa kurejesha mkopo.

Kuhusu kutoa mikopo imebainishwa kuwa Mkurugenzi wa Manispaa atakuwa na wajibu wa kuhakikisha wilaya inatenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo hiyo.

Aidha, mikopo inatolewa kwa kuzingatia masharti ya kanuni hizo na kwamba vikundi vilivyokopeshwa vinarejesha mikopo kwa wakati.

Kadhalika, inabainisha kuwa mgao wa fedha za mikopo unapaswa kufanywa  kwa kuzingatia masharti ya kanuni  na itatolewa  kwa kuzingatia mgawo wa kiasilimia.

Vikundi vya vijana, wanawake na wenye  mahitaji maalumu.

 Jambo lenye neema ni kwamba mikopo itakayotolewa chini ya kanuni hizo haitotozwa riba. 

Wakati sifa za kupata mkopo zinabainishwa kuwa kikundi cha wanawake, vijana au watu wenye ulemavu kitakuwa na sifa ya kupata mkopo endapo, kimesajiliwa. 

 Kanuni zinabainisha kuwa kikundi kinapaswa kujishughulisha na ujasiriamali au kinakusudia kuanzisha shughuli za ujasiriamali mdogo au wa kati.

Kwa kikundi cha wanawake au vijana kiwe na idadi ya wanakikundi kuanzia 10 na kuendelea na kwa wenye mahitaji maalumu idadi ya wanakikundi isipungue watano na isiyozidi 10.

Pia  kikundi kiwe na akaunti ya benki iliyofunguliwa kwa jina la kikundi kwa ajili ya matumizi ya kikundi na wanachama wake ni raia wa Tanzania wenye akili timamu na umri zaidi ya miaka 18.

Naamini kwamba serikali za mitaa pamoja na kuwa wametingwa na maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, bado wataona umuhimu wa kuwajibika kwa wanufaika kuhusu mikopo.

Ni kwa kutoa tangazo kwa umma kwa madhumuni ya kuutarifu na vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuhusu fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo yao.