Wiki ya Huduma kwa Wateja itoe funzo

Nipashe
Published at 12:12 PM Oct 09 2024
Wafanyakazi wa NSSF katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Picha:Mtandao
Wafanyakazi wa NSSF katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja.

TAASISI mbalimbali nchini na duniani kwa ujumla zinaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja. Katika kuadhimisha wiki hii, taasisi mbalimbali zinaonesha shughuli mbalimbali kuwahudumia wateja katika maeneo mbalimbali pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma na kazi zinazofanya.

Katika kuonesha umuhimu wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, wakuu wa taasisi wakiongozwa na maofisa watendaji wakuu, wakurugenzi, mameneja na maofisa wote mpaka wafanyakazi wa ngazi za chini, wako mstari wa mbele kuwahudumia wateja na kuwaeleza shughuli na huduma zinazotolewa katika kampuni na mashirika hayo.

Mara nyingi, wakati wa kuadhimisha wiki hii, imeshuhudiwa wakurugenzi watendaji wa benki, mathalan, wakiwa kwenye madirisha ya kutoa huduma. Yote hiyo ni kuonyesha umuhimu wa huduma kwa wateja, ikiwa pia njia ya kushawishi wale wasiotumia huduma au bidhaa zao kujiunga na taasisi hizo ili kunufaisha pande zote.

Wakati wiki hii ikiadhimishwa, kumekuwa na maalamiko kwa baadhi ya wateja na wadau kuwa zimo taasisi ambazo zinasherehekea wakati huduma zake ni za viwango duni au kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma. Moja ya taasisi hizo ni za huduma za maji.

Moja ya taasisi hizo imewatakia wateja wake maadhimisho mema ya wiki ya maji na wateja kutoa maoni mbalimbali kwenye makundi sogozi wakihoji viongozi na watumishi wa taasisi hiyo wanajisikiaje wanapoadhimisha wiki hii adhimu wakati wananchi wanalalamikia kukosa maji?

Kutokana na hoja hiyo, viongozi wa serikali wenye dhamana katika sekta hiyo na watendaji wa mamlaka wameibuka na kutoa ufafanuzi kuwa kuna kasoro za kifundi na zingine ziko nje ya uwezo wao katika kuwafikia wateja, hivyo kuomba radhi kwa wale wanaokwazwa na hali hiyo. Kwa kutoa maelezo hayo, wamedhihirisha ule msemo kwamba muungwana ni kitendo.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka kwa taasisi kufanya mambo mbalimbali. Kwa taasisi zilizo makini, hutumia maadhimisho hayo kufanya tathmini ya mafanikio, kasoro na upungufu katika utoaji wa huduma.

Pale penye mafanikio, hupongezana na pia kuangalia ni namna gani ya kuongeza viwango katika utoaji wa huduma ili kuvutia wateja zaidi. Aidha, pale panapojitokeza kasoro au kutofikiwa malengo yaliyokusudiwa, hujiuliza sababu na kuchukua hatua stahiki ili kuziondoa na hatimaye kuboresha viwango vya huduma.

Miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wateja, ni huduma mbovu ikiwamo lugha mbaya kwa wateja, kutokuwapo mazingira rafiki ya utoa huduma na viwango vinavyotolewa kuwa vya hali ya chini.

Katika hoteli kwa mfano, imekuwa ikielezwa kuwa huduma zinazotolewa katika tasnia hiyo ni za viwango vya duni hatua ambayo huwakimbiza wateja wengi. Mteja tangu kuingia, hukaribishwa isivyostahili na hiyo imesababisha hoteli nyingi kuanzishwa kwa kishindo na kuporomoka viwango na hatimaye kufungwa kwa muda mfupi.

Hata katika baadhi ya hospitali, kumekuwa na malalamiko kuwa huduma zinazotolewa si rafiki kwa wagonjwa. Baadhi ya wauguzi, kwa mfano, wamekuwa wakidaiwa kutoa lugha chafu kwa wagonjwa au kutoa huduma kwa kusuasua jambo ambalo wakati mwingine husababisha vifo ambavyo vinaweza kuzuilika.

Kwa jumla, Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka huu, itoa fundisho kwa taasisi kujipanga upya katika utoaji huduma ili kupaa katika viwango vyao badala ya kufanyika kila mwaka kwa mazoea.