Ngao ya Jamii kumalizika bila kujua ligi itaanza lini ni kituko

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:37 AM Oct 07 2024
JKT Queens wakishangilia kutwaa ngao ya jamii.
Picha:Mtandao
JKT Queens wakishangilia kutwaa ngao ya jamii.

NIWAPE kwanza hongera timu ya JKT Queens kwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Yanga Princess bao 1-0, katika mchezo wa fainali uliopigwa Jumamosi Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Kwa jinsi walivyocheza wakianza kwa kutoa kipigo kizito cha mabao 7-0 dhidi ya Ceasiaa Queens katika mchezo wa nusu fainali walionekana kustahili ubingwa huo.

Ikumbukwe mwaka jana JKT Queens ilifungwa kwenye hatua ya fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4 na Simba Queens, baada ya sare ya bao 1-1.

Msimu huu Simba Queens ilitolewa hatua ya nusu fainali na watani zao wa jadi, Yanga Princes kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya sare ya bao 1-1.

Baada ya hongera, nitoe pongezi pia kwa timu zote nne zilizoshiriki michezo hiyo ya nusu fainali, fainali na kusaka mshindi wa tatu kwa kutoa burudani kwa mashabiki ambao walikuwa wakimiminika kwenye uwanja huo uliopo Mwenge Dar es Salaam, kwa ajili ya kuangalia michezo hiyo.

Wakati michezo hiyo inapigwa, nilifuatilia na kugundua kuwa hakuna taarifa yoyote ya ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake mpaka sasa.

Hata Kocha Msaidizi wa Ceasiaa Queens, Shabani Zanziba, alisikika akisema baada ya Ngao ya Jamii kutakuwa tena na mapumziko kabla ya kuanza ligi hiyo.

Cha kujiuliza mpaka sasa ni kwa nini hakuna ratiba yoyote ya Ligi Kuu ya Wanawake, wakati mechi za Ngao ya Jamii zimechezwa.

Maana ya Ngao ya Jamii, ni kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi kokote kule, lakini hii imekuwa kinyume chake.

Imeonekana kama Ngao ya Jamii ni kama michuano tu ambayo inajitegemea na haiashirii chochote kile.

Kwa upande wa soka la Wanaume tunaona kuwa ikichezwa Ngao ya Jamii tayari ratiba ya Ligi Kuu nayo inakuwa imeshatoka.

Msimu huu baada ya kumalizika kwa Ngao ya Jamii tu, Agosti 11 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ilipoichukua kwa kuifunga Azam FC mabao 4-1, siku tano baadaye tu, yaani Agosti 16, Ligi Kuu Tanzania Bara ikaanza.

Sijajua tatizo ni nini, lakini kama hali ni hivi, nadhani kusingekuwa na haraka ya kuanza mechi za Ngao ya Jamii. Nadhani ingesubiriwa hadi mipango ya ligi hiyo ikae sawa.

Kwa maana hiyo, klabu zilikusanya wachezaji na kuwaweka kambini kwa ajili ya michezo miwili tu ya Ngao ya Jamii, na baada ya hapo zitalazimika kuvunja kambi hadi hapo zitakapopata taarifa ya kuanza kwa Ligi Kuu.

Hakuna kitu kingine unachoweza kukiita, ila ni usumbufu na kituko. Huu ulikuwa ni wakati wa wachezaji kuendelea kukaa kambini na kujifua kwa ajili ya kujiandaa na ligi. Ikumbukwe kuwa hakuna klabu yoyote inayoweza kuwaweka kambi wachezaji eti ikijiandaa na Ligi Kuu ambayo haijuu itachezwa lini, labda JKT Queens tu.

Na hiyo ni kwa sababu yenyewe ni timu ya jeshi, ambayo muda wote wapo kambini na mazoezi ni kama kazi za kawaida tu, na hawana tatizo la gharama.

Kwa klabu zingine kwa kuepuka gharama zitawaacha wachezaji waende makwao mpaka watakapowaita tena. Baadhi yao ni wachezaji kutoka nje ya nchi, hivyo watarejea makwao wakati tayari walikuwa wameshafika kwenye maeneo ya kazi.

Ifike wakati sasa wahusika, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), chini ya vitengo vyake zinavyosimamia soka la wanawake kuangalia hili.

Wanapaswa kuandaa Ngao ya Jamii ambapo tayari wameshajiandaa na Ligi Kuu ya Wanawake na si hivi ilivyotokea msimu huu.