Waamuzi acheni woga wa kuongeza dakika soka lichezwe kwa dakika 90

Nipashe
Published at 10:32 AM Oct 07 2024
Mwamuzi Jonesia Rukyaa
Picha:Mtandao
Mwamuzi Jonesia Rukyaa

KATIKA mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Coastal Union, uliochezwa Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, kuliibuka mzozo kwa wachezaji kumzonga mwamuzi kwa kitendo chake cha kumaliza mpira wakati wakiamini ulikuwa unastahili dakika zaidi za kuendelea kucheza.

Hali hiyo ilisababisha tafrani kidogo, ambapo alizongwa na wachezaji wa pande zote mbili pamoja na mabenchi yao ya ufundi, kila upande ulionekana kutoridhishwa na namna mpira ulivyomalizika, wote wakiamini dakika zilipaswa kuongezwa kutokana na matukio mbalimbali yaliyosababisha mpira kusimama na kutochezwa kwa dakika zote 90.

Coastal Union wao waliona kama shambulizi lao limezimwa kwa makusudi kwani walikuwa wanagongeana kwenda langoni mwa Simba.

Simba nao waliona dakika zilikuwa bado, walizihitaji kwa kile walichoona wangeweza kupata bao la tatu katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Nipashe tunaona uhitaji huo wa dakika kwa timu zote mbili unaweza kuanza kuwaamsha waamuzi wengi wa Kitanzania hasa wa akiba ambao wana matatizo ya kutotunza muda kwa usahihi.

Katika mchezo huo, Coastal Union walionekana kupoteza dakika nyingi kwa makusudi baada ya kurudisha mabao mawili.

Kwa bahati nzuri wao walijua hilo, lakini baadaye walizihitaji baada ya kuona wameweza kuwamudu wapinzani wao, Simba ambao nao walijua Coastal walipoteza sana muda, hivyo waliuhitaji ili wasake bao la ushindi.

Tatizo la kuongezwa dakika chache ambazo hazina uhalisia kwa sasa limeonekana kuota mizizi kwenye soka la Tanzania.

Kwanza kabisa ni nadra sana kuona zimeongezwa dakika tano kipindi cha kwanza. Mara nyingi kipindi cha kwanza ndicho huongezwa dakika chache zaidi hata kama mpira ulisimama kwa dakika tano kutokana na matukio tofauti uwanjani, lakini kwa Ligi Kuu nchini, waamuzi huongeza dakika mbili au tatu tu.

Kipindi cha pili ndiyo angalau unaweza kuona zimeongezwa nne, zikizidi sana tano. Hii imekuwa ni kama utaratibu au kanuni za waamuzi wa Ligi Kuu na haijulikani wao wanaendeshwa na kanuni zipi tofauti zile za Shirikisho la Soka duniani (FIFA), ambazo zinataka kuhakikisha mechi inachezwa ndani ya uwanja kwa dakika 90.

Hata kama kutakuwa na mapumziko ya kunywa maji, wachezaji kuumia na ucheleshwaji wa muda makusudi, lakini bado baadhi ya waamuzi hapa nchini wamekuwa hawaongezi dakika stahiki zilizopotea.

Kwa sasa Ulaya tunaona, zinaongezwa kuanzia dakika tano mpaka 10, kutegemea na upotezwaji wa muda. Hii yote ni kutaka mpira uchezwe ndani ya uwanja kwa dakika zote 90 na si chini ya hapo. 

Kule Ulaya wanapoongeza mpaka dakika 10, timu huwa hazipotezi muda, cha kushangaza hapa nchini ambapo timu zinazoitwa au kujiita ndogo zikicheza na Simba au Yanga, halafu zikiwa na uhakika fulani tu kama mechi hii kushinda ama kupata sare kunakuwa na vituko vya wachezaji kujilaza makusudi, makipa kujifanya wameumia hadi kuvua 'gloves' na viatu, lakini mwamuzi mtunza muda ataongezwa tatu au nne tu.

Lakini pia waamuzi wa ndani nao wamekuwa waoga kuongeza dakika baada ya zile za nyongeza hata kama zilizoongezwa mpira hazikukamilika kwa mpira kuchezwa uwanjani kutokana na upotezwaji huo wa muda.

Sisi tunaona ifike wakati sasa waamuzi waondoe woga, wachezeshe kwa dakika zote 90 kwa mujibu wa kanuni za Fifa. Hata zikiongezeka dakika 10, kama refa atachezesha kwa haki na kufuata sheria za soka tunaamini hakuna matatizo.