DAWASA iseme kweli kuhusu ukosefu huduma ya maji Dar

Nipashe
Published at 09:40 AM Oct 03 2024
DAWASA iseme kweli kuhusu ukosefu huduma ya maji Dar
Picha: Mtandao
DAWASA iseme kweli kuhusu ukosefu huduma ya maji Dar

KWA takriban mwezi sasa, wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani hususan Kibaha, wanapata shida ya maji hatua inayowafanya wapate adha kubwa ya kusaka huduma hiyo huku wengine wakitumia maji yasiyo salama kwa afya zao ambayo yanauzwa kwenye madumu na hayajulikani yanakotoka wapi.

Katika maeneo mbalimbali kama vile Tabata Segerea, Ubungo, Sinza, Kijitonyama, Saranga, Malamba Mawili, Kinyerezi, Kimanga na Kisukulu, ni jambo la kawaida kukutana na watu wakiwa wamebeba ndoo kichwani na wengine wakiwa na madumu kwenye mikokoteni. Yote hiyo inaonesha kuwa kuna tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.  

Pamoja na kwamba tatizo hilo limekuwa kubwa hivi sasa, wananchi katika baadhi ya maeneo wamebainisha kwamba tatizo hilo liko kwa zaidi ya mwezi sasa na limesababisha watumie muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za uzalishaji. Wako wengine ambao wamesema wanalazimika kuamka saa 11:00 alfajiri Kwenda kutafuta maji katika visima au kuvizia kama yanaweza kutoka hali ambayo inawaweka katika mazingira ya hatati ya kufanyiwa ukatili.  

Katika eneo la Saranga wilayani Ubungo, kwa mfano, wananchi wamelalamika kuwa tatizo hilo kwa sasa ni sugu kwa kuwa wamekosa huduma hiyo kwa zaidi ya mwezi na wanapouliza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), hakuna majibu sahihi yanayotolewa zaidi ya kusema wavute subira huduma itarejea wakati wowote. Wakati maofisa wa DAWASA wakijibu hivyo, wananchi wanakumbwa na mshangao kwa sababu kuna wakati maji hayapatikani lakini mabomba barabarani yanatoa maji kutokana na kuwa yameharibika.  

Eneo la Segerea ni mojawapo ya sehemu zilizokumbwa na tatizo hilo, huku kama ilivyo kwa wananchi wa Saranga, majibu yanayotolewa na watendaji wa mamlaka hayo si ya kutia matumaini ya kupata huduma hiyo. Wananchi hao wamekuwa wakisaka maji kutoka sehemu moja kwenda nyingine huku wakitegemea kununua maji kutoka kwa wauzaji kwenye madumu au visima vya watu binafsi.  

Hali hiyo ya kukosekana kwa maji inakwenda kinyume cha matumaini yaliyokuwa yakitolewa na watendaji wa DAWASA waliyokuwa wakiyatoa hivi karibuni kwamba wameongeza kasi ya usambazaji wa huduma kwa wananchi huku wakijinasibu kuwa wananchi hadi wa pembezoni kama vile Mabwepande, Mpigi Magohe na Mbezi Msakuzi tayari wamefikiwa na huduma hiyo. 

Kama kasi ya usambazaji wa huduma hiyo imeongezeka kutokana na uwekezaji wa mabilioni ya shilingi katika miradi ya maji mkoani Dar es Salaam na maeneo ya Pwani ni kubwa, iweje sasa wananchi wahangaike kupata huduma hiyo na kuyatafuta kwa tochi? 

Kwa namna ilivyo sasa, kuna shida mahali ambayo pengine ni kubwa na haisemwi hadharani. Mazingira yanaonesha hivyo kwa sababu Juni 30, mwaka huu, Waziri wa Maji Aweso alifanya ziara katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Dar es Salaam, katika ziara hiyo, alishuhudia madudu yaliyosababisha aliyekuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Kiula Kingu, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa mamlaka hiyo, Shaaban Makwenywa, kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.  

Wakati wa ziara hiyo, Aweso alitembelea Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Mbezi, Mshikamano na Tegeta A alikoshuhudia matangi ya maji yakiwa hayana maji, hivyo kusababisha wananchi kutokupata huduma hiyo bila sababu zozote za msingi. 

Katika mtazamo chanya, liko tatizo ndani ya DAWASA ambalo lazima linatokana na utendaji wa wafanyakazi na uongozi mbovu au tatizo la kifedha linaloikumba kiasi cha kushindwa kutimiza azma yake ya kuwapatia wananchi huduma ya maji ya uhakika. Lakini kama ni ukosefu wa fedha, mbona wananchi wanalipa tena wale wasiotimiza hilo wanakatiwa maji.  

Ni vyema serikali kupitia Wizara ya Maji, yenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo mijini na vijijini, ikichukua hatua madhubuti kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.