Vijana wamjue, kumwiga Sokoine

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:06 AM Oct 02 2024
Edward Moringe Sokoine.
Picha: Mtandao
Edward Moringe Sokoine.

MIAKA 40 iliyopita, Aprili 12, 1984 taifa lilimpoteza Edward Moringe Sokoine, mmoja wa viongozi bora wanaoendelea kuheshimika hata leo.

Alifariki kwa ajali ya gari iliyotokea Dakawa mkoani Morogoro, akiwa safarini kutoka Dodoma kurejea Dar es Salaam, baada ya kikao cha bunge.

Miongo minne ni muda mrefu, hivyo  ni wazi kuwa mamilioni ya Watanzania hasa vijana hawamfahamu Sokoine.

Sokoine ambaye angekuwa hai leo angekuwa na miaka 86, alizaliwa Agosti 1, 1938, katika kitongoji cha Kilasho kilichoko  kijiji cha Emairete wilaya ya Monduli mkoani  Arusha.

Ni miongoni mwa viongozi wachache wakati huo wasomi akisoma katika Sekondari ya Umbwe, iliyoko mkoani Kilimanjaro na kubwa zaidi alikuwa mpigania uhuru jasiri akijiunga na TANU,  miezi kadhaa kabla ya uhuru 1961.

Kwa vijana ambao hawamjui Sokoine ambaye, kitabu kinachozungumzia maisha yake kilizinduliwa jana jijini Dar es Salaam, wafahamu kuwa alikuwa anaipenda Tanzania na mtetezi wa wanyonge.

Mathalani, anaelezwa kuwa alipoapishwa kuwa mbunge wa jimbo la Maasai, cha kwanza alipoingia bungeni anahoji hatima ya Wamasai, akiuliza haya:

"Inakuwaje  Wamasai wa Ngorongoro wanakatazwa kulima, wakati hawana mifugo wala kitu cha  kuwapatia chakula?"

Kadhalika anawaambia wabunge wapasue vichwa, akisema tangu uhuru yapo makabila yamefikia  maendeleo makubwa lakini  mengine yapo nyuma akitaka maelezo ya  serikali kuwaelimisha walioko nyuma kimaendeleo ili walingane na wengine waliosonga mbele zaidi.

ALichokuwa akikitazama ni Wamasai na Watanzania wengine ambao hawakuwa na barabara, shule, maji safi, umeme na hospitali.

Kwa masuali yake hayo na mengine inaonyesha kuwa Sokoine alipenda usawa na ulinganifu kwenye maendeleo.

Alichukia umaskini tena ndani ya taifa ambalo lina rasilimali nyingi kama Tanzania. Alikuwa mzalendo ambaye tangu mwanzo alitamani maisha ya viongozi na raia yawe ya kiuadilifu na yasiyosujudu ubinafsi.

Vijana wasiomjua Sokoine wajifunze kupenda vyao na kuipenda nchi yao na nyumbani kwao pia. Hasa vijijini wanapotoka.

Sokoine anaelezwa kuwa akiwa  miaka 27 aligombea na kushinda ubunge jimbo la Masai na kuazimia kuleta mabadiliko.

Kwa angalizo hilo vijana nao wabadilike wasiendelee kuogopa kupiga kura na kushiriki shughuli za kisiasa hasa uchaguzi wa serikali za mitaa ulio mbele yao.

Utawasikia wakijidanganya kuwa hawawezi kupigakura maana siasa haiwahusu huko ni kukosa mwamko wa kisiasa.

Ni lazima kujituma na kushiriki mikutano ya kisiasa, vijijini kwenye vitongoji, mitaa na katika masuala yote yanayohusu maendeleo.

Pamoja na mambo mengine Sokoine anasifika kwa kuchapakazi hadi Mwalimu Nyerere na timu nzima ya TANU  mwaka 1972 ikiona anafaa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, akipewa majukumu makubwa kitaifa.

Mwaka 1977 anakuwa Waziri Mkuu wa Tanzania ni  kutokana na utendaji kazi wake makini, ambao vijana wanatakiwa kuuiga leo.

Baadhi ya vijana wa sasa hawapendi kujituma hata shuleni wanatamani watu kuwafanyia mitihani.

Wengi wanapendelea kufanyiwa kila kitu kuanzia mawazo  kwa sababu idadi kubwa si wabunifu, lakini pia siyo watu wa kutafuta maarifa wala kuchangamka ili kubadili maisha yao.

Kuna mamia ya vijana wako kwenye vituo vya mabasi mfano jijini Dar es Salaam, wakiwabughudhi abiria kuwauliza iwapo wanakwenda mikoani wawapeleke kwenye mabasi ya mikoani.

Wapo wengine maelfu wanapiga debe stendi kuita abiria wanaokwenda maeneo mbalimbali wakijiita wapigadebe.

Wapigadebe wanapiga kelele vituoni wakati mabasi yameandikwa yanapokwenda, yote hayo ni kutokupenda kufanyakazi.

Vijana badilikeni na kumuiga Sokoine kwa kufanyakazi na kujihusisha na shughuli rasmi zinazojenga maisha yenu, ya jamaa zenu hasa nyumbani vijijini mnapotoka.

Sokoine hakulala kwa ajili ya kubuni mbinu, kupanga mipango ya kuiletea Tanzania maendeleo, vijana wa leo mara ngapi wanakesha wakitafuta mbinu za kujiondoa kwenye umaskini na kufikia hali bora za maisha yajayo?

Ni vizuri kujitafuta na kujipata ili kuwa sehemu ya watu wanaoacha alama kwenye maisha yako na ya wengine kama alivyofanya Sokoine.