Sungusungu wanaojifanya mahakama, hiyo haikubaliki

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:29 AM Oct 04 2024
Mahakama.
Picha:Mtandao
Mahakama.

KUMEKUWA na tabia ya baadhi ya walinzi jadi, maarufu kama sungusungu kwenye mikoa mbalimbali nchini kufanya kazi zisizowahusu, ambazo sizo wanazotakiwa kufanya.

Walinzi hao ambao mijini wanajulikana kama Polisi Jamii, baadhi ya mikoa wamekuwa wakifanya kazi ya kukamata wahalifu lakini hao hao pia wamekuwa wakijifanya mahakama na kutoa adhabu. 

Hiki kimekuwa ni kilio kikubwa kwa wananchi wanaokutana na adha hiyo, ambapo pamoja na mambo mengine wamekuwa wakikutana na adhabu kubwa kuliko kosa walilolifanya, kutengwa na jamii na adha zingine zinazofanana na hilo.

Jeshi hilo la Sungusungu limeanzishwa kwa sababu ya kulinda usalama wa raia na mali zao, kusaidia maeneo kuwa na amani na utulivu, kuzuia uhalifu, lakini wanapowakamata au kukuta kuna uhalifu wanatakiwa kuwaona askari polisi, au kuwapeleka kituoni wahalifu. 

Matokeo yake, baadhi yao ambao si waaminifu wamegeuza kuwa mradi kwani wanawaadhibu watu kwa kuwapiga faini mifugo kama mbuzi, ng'ombe, mazao, wakitumia bakora, au kuwaambia wanakijiji wamtenge kwenye shughuli za kijamii na yoyote atakayekiuka naye ataadhibiwa. 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, ameliona hili na kulikemea vikali. Alizungumza katika mkutano wa hadhara juzi kwenye kijiji cha Manyanda mkoani Shinyanga, alisema kumekuwa na tabia ya sungusungu kutoa adhabu kwa wananchi ikiwamo kuwatenga kutojihusisha na chochote ndani ya jamii.

 Akasema kwa mujibu wa sheria za nchi, jukumu la kutoa hukumu ni la mahakama pekee na si mtu yeyote.

 Alisema serikali inatambua mchango wa jeshi hilo la jadi sungusungu la kuhakikisha amani na utulivu utawale ndani ya jamii na kudhibiti vitendo vya kihalifu, lakini wanapokuwa katika majukumu yao, wahakikishe wanazingatia sheria za nchi.

Binafsi nampongeza mkuu wa mkoa huyo, na alichokisema hakipo kwenye kijiji hicho au mkoani mwake tu, bali mikoa mingi na vijiji vingi nchini.

Haiwezekani mtu anayekamata ndiyo anayetoa hukumu na adhabu. Ndiyo maana utaona hata askari polisi wakikamata wahalifu wanawapeleka mahakamani, siyo wao wanaowahukumu, ndipo kuna chombo cha kutafsiri hukumu. Na hata mtu akihukumiwa siyo mahakama inayomweka kwenye magereza yake. Mahakama haina magereza, bali kuna Jeshi la Magereza, ambalo nalo liko kivyake. Yenyewe inapewa tu mtu ambaye amehukumiwa.

Hapo utaona kuna taasisi tatu tofauti na hii yote ni kumfanya yeyote awe na haki, na kuzuia visasi, chuki na kukomoana. Waliokaa kutengeneza mfumo huo hawakufanya hivyo kwa bahati mbaya.

Binadamu anatakiwa kuhukumiwa kutokana na uzito wa kosa alilolifanya, sungusungu wanatoa adhabu kubwa kwa kosa dogo tu, pia adhabu siyo kumkomoa mtu, bali ni kumkumbusha kuwa alichokifanya si sahihi, ndiyo maana mahakimu hutoa adhabu kulingana na kosa alilofanya mtuhumiwa na si vinginevyo.

Nadhani kuanzia sasa sungusungu wenye tabia hii wamulikwe na kuchukuliwa hatua ili raia wakae kwa amani na utulivu kwenye nchi yao huru.