Heshima pekee kwa wazee ni kuwajali, kuwapa haki zao

Nipashe
Published at 09:00 AM Oct 02 2024
Heshima pekee kwa wazee ni kuwajali, kuwapa haki zao
Picha: Mtandao
Heshima pekee kwa wazee ni kuwajali, kuwapa haki zao

TANZANIA jana iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani. Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka kutokana na Azimio Na.45/106 la Umoja wa Mataifa ambalo lilitenga Oktoba Mosi, kila mwaka kuwa siku ya Kimataifa ya Wazee na kuanza rasmi mwaka 1991.

Tangu kuanzishwa kwa siku hiyo, Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuadhimisha lengo likiwa kuhakikisha jamii inajengewa uelewa na kutiwa hamasa kuhusu kulinda haki, ustawi na maslahi ya wazee. 

Mbali na lengo hilo, jamii pia, hasa wale ambao hawajafikia hatua ya uzee, hukumbushwa na kutambua kuwa uzee hauepukiki na kila anayeomba na umri mrefu anaombea kufikia uzee na hakika, anaombea afikie uzee mwema, hivyo hana budi kumpenda na kumheshimu mzee wa leo. Kwa maneno mengine, jamii inakumbushwa kuwa watoto, vijana na watu wa makamo wa leo ni vijana wa kesho, hivyo wasiwadharau, kuwanyanyasa hata kuwanyanyapaa wazee. 

Kama kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2024 inavyosema “Tuimarishe Huduma kwa Wazee, Wazeeke kwa Heshima”, kundi hilo linastahili heshima kwa kuboreshewa mifumo yao, ikiwamo upatikanaji wa huduma mbalimbali kama vile afya, malazi na makazi bora, ulinzi na usalama. 

Katika kutimiza azma hiyo, kila mdau ana wajibu wa kufanya yale yanayopasa. Serikali kwa upande wake, inapaswa kuhakikisha wazee wanapatiwa matibabu kwa kutengewa dirisha maalum pamoja na bima ya afya, kuwapo kwa sera ya wazee inayoendanaa na wakati wa sasa. 

Pia inafahamika kwamba wazee ni kundi ambalo limetoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa, hivyo linapaswa kupewa kipaumbele katika huduma mbalimbali. Aidha, kumekuwa na changamoto zinazowakabili wazee kama vile malipo ya pensheni baada ya kustaafu na pia kucheleweshwa mafao yao baada ya kustaafu kuhu baadhi ya maofisa wa mifuko ya jamii wakiwazungusha na kutengeneza mazingira ya kutaka watoe rushwa ndipo watimizie haki zao. 

Jamii, kwa maana ya watu walio karibu na wazee hao pamoja na ndugu na jamaa, wanapaswa kuwalea wazee kwa misingi iliyo bora ili waendelee kuishi badala ya kuwanyanyasa hata kuwafanyia vitendo vya unyama vikiwamo mauaji kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa katika baadhi ya maeneo.

Ni jambo la kutia moyo kwamba serikali katika taarifa yake kuelekea kwenye maadhimisho hayo, ilisema katika kuboresha mifumo mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wazee, iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha kuhuisha Sera ya Wazee. Kuhuishwa kwa sera hiyo ni dhahiri kwamba ni hatua ya kuelekea  kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kundi hili ambalo ni tunu ya taifa. 

 Ahadi hiyo ya serikali inaleta matumaini kwa wazee kwamba matatizo na changamoto ambazo wamekuwa wakipitia hata wengine kukumbwa na maradhi yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya moyo, kisukari na figo ambayo yanasababishwa na msongo wa mawazo kwa sababu ya kusotea mafao yao, zitapungua kiasi kikubwa. 

Hali hiyo itafikia hivyo kwa kuwapo mifumo stahiki kuhusu wazee, kutawaondolea changamoto hizo ambazo pia husababisha kupoteza maisha kutokana na mambo ambayo yanaweza kutatulika. 

Mbali na matatizo hayo, wazee pia wamekuwa wakilalamika kutoshirikishwa kikamilifu katika mipango ya maendeleo, kukosa jukwaa la kutoa mawazo yao hasa katika jamii jambo ambalo pia huwasababishia sonona na msongo wa Mawazo kuona kwamba wamedharauliwa. Jambo hilo pia linapaswa kuangaliwa kwa upana ili wasijione wametengwa huku jamii ikitambua wazee bado ni muhimu katika kutoa ushauri wa mambo mbalimbali yanayohusu jamii hasa kutokana na uzoefu wao, ndiyo maana kukawa na msemo kwamba uzee ni dawa. 

Serikali pia ifikirie kutoa nafasi za upendeleo kwa kundi la wazee katika vyombo vya uamuzi kwa kuwa na wawakilishi kama ilivyo kwa makundi ya wanawake na wenye ulemavu. Kwa kufanya hivyo watajiona wanajaliwa na kuheshimiwa.