Kabudi aonya matumizi mabaya ya 4R kuingilia mamlaka, uamuzi

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 12:08 PM Oct 10 2024
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, ameonya matumizi mabaya ya dhana ya 4R za Rais Samia Suluhu Hassan, kutumika kama kichaka cha watu kufanya mambo yanayovunja sheria za nchi, ikiwamo kuingilia mamlaka ya vyombo vya uamuzi.

Prof. Kabudi alisema hayo jana jijini hapa wakati akifungua kikao cha Menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Alisema watu hawapaswi kutumia vibaya dhana hiyo ya Rais kwa kufanya mambo ambayo yanavunja sheria na kufikiri kuwa wanayo haki ya kufanya jambo ambalo linaweza kuingilia uhuru wa vyombo vya uamuzi.

“Dhana hii ya 4R isiwe kichaka cha watu kufanya mambo ya fujo na kuingilia mamlaka za vyombo vya uamuzi na kuvunja sheria za nchi bali itumike kwa misingi iliyokusudiwa bila kuhatarisha umoja wetu na kuzingatia hadhi ya kila mmoja wetu,” alisema Prof. Kabudi.

Alisema taasisi hizo tatu zinapaswa kufanya mambo yao kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni bila ya kuathiriwa na mihemuko ya kundi au mtu fulani.

Pia alizitaka taasisi zote zilizopo katika masuala ya haki jinai nchini, kuimarisha weledi katika shughuli zote za upelelezi ili kumaliza tatizo la mrundikano wa mashauri na mahabusu gerezani.

Alisema moja kati ya changamoto zinazochangia ongezeko la mrundikano wa mashauri pamoja na mahabusu, ni kasi ndogo ya upelelezi, hivyo ipo haja taasisi zote zinazohusika na haki jinai kuongeza ufanisi kumaliza hali hiyo.

Vilevile, aliwataka kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara ili kufahamiana na kila mmoja kujua majukumu yake yanaishia wapi na ya mwenzake yanaanzia wapi, ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri na kutoa haki kwa wakati.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani, Prof. Kabudi, aliagiza Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, TAKUKURU na Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kusimamia sheria ili uchaguzi huo uwe huru na wa haki.

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa na mwakani 2025 ni uchaguzi mkuu niwaombe msimamie sheria za uchaguzi, ili nchi yetu kuendelea na utulivu na amani iliyopo na kuepuka mambo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika mataifa mengine,” alisema.

Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Sylvester Mwakitalu, alisema kikao hicho kinachokutanisha ofisi zinazounda utatu katika masuala ya haki jinai nchini, lengo lake ni kujadili changamoto mbalimbali katika sekta hiyo pamoja na kuandaa mikakati ya kupata suluhu.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, alisema tangu kuanzishwa kwa umoja wa taasisi hizo, kasi ya uendeshaji mashauri imeongezeka na kusaidia kupunguza mrundikano wa mahabusu katika magereza.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya miaka mitatu iliyopita kuhusu utolewaji wa haki jinai nchini, ilifichua udhaifu mkubwa katika eneo hilo. Ndiyo chanzo cha Rais Samia kuunda tume ya kuishauri serikali hatua za kuchukua kuondoa dosari zilizoibuliwa na mdhibiti.