Red Cross wasambaza vijana wao kukabili Mpox

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 01:29 PM Oct 10 2024
Samwel Katamba katikati akizungumzia hatua ya kupeleka wafanyakazi wa kujitolea. Kulia ni Christian na Maudline Tarazo.
Picha: Sabato Kasika
Samwel Katamba katikati akizungumzia hatua ya kupeleka wafanyakazi wa kujitolea. Kulia ni Christian na Maudline Tarazo.

CHAMA cha Msalaba Mwekundu Tanzania, kimeungana na serikali kudhubiti ugonjwa wa Mpox mikoa ya mpakani mwa nchi jirani, kwa kupeleka wafanyakazi 750 wa kujitolea ili watoe elimu kwa wananchi.

Elimu hiyo inahusu kutambua dalili za ugonjwa huo, jinsi ya kujikinga na hata kupata matibabu. Hayo ni kwa mujibu wa Meneja wa kukabiliana na maafa wa chama hicho, Samwel Katamba.

Amesema hayo Dar es Salaam wakati akielezea hatua ya chama hicho kupeleka wafanyakazi wa kujitolea kwenye baadhiya mikoa ikiwamo ya Rukwa, Mbeya, Katavi, Songwe, Mara, Kigoma, Mwanza na Kagera.

"Vijana wetu wanashirikiana na watu wa huduma ya afya ngazi ya jamii wanatoa elimu nyumba kwa nyumba, katika magari, shuleni  na katika mikusanyiko ya watu ili wajue dalili za ugonjwa," amesema Katamba.

Amefafanua kuwa Tanzania sio kisiwa, bali imepakana na baadhi ya nchi zenye changamoto ya magonjwa ya mlipuko ukiwamo wa Mpox, ndio maana wamepeleka wafanyakazi hao ili wakatoe elimu.

Ofisa wa Maafa wa chama hicho, Christa Chrisstian ametaja moja ya majukumu ya RED CROSS ni kukabiliana na majanga, na kwamba mlipuko wa Mpox ni moja ya mjanga yanayohitaji kukabiliwa

"Wizara ya Afya inasema ugonjwa huo haujaingia nchini, lakini suala la kuchukua tahadhari ni la muhimu, ndio maana tumeweka wafanyakazi wetu wa kujitolea wasaidie kuelimisha jamii ili iwe uelewa wa kutosha na kuchukua tahadhari," alisema Christa.

Mtaalam wa saikolojia wa RED CROSS, Maudline Tarazo, amesema, watu wanapokumbwa na majanga au magonjwa, wengine hukata tamaa, na kufafanua kuwa huwa kinawaweka sawa watu wa aina hiyo.

"Vilevile, tunawalekeza kila kupiga simu namba 0800750150 iwapo atahisi kuwa na dalili za ugonjwa huo ili hatua zichukuliwe haraka, kwani namba hiyo inapigwa bure," amesema Maudline.

Maudline alisema RED CROSS imejaa wataalam wa fani mbalimbali ambazo huzitumia wakati wa majanga mbalimbali, yakiwamo ya ajali, mafuriko, magonjwa na hata ukame na kimbunga.