"Wakazi Dar es Salaam ya Kusini uhakika Majisafi ni Desemba 2024"

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:25 PM Oct 10 2024
Wakazi Dar es Salaam ya Kusini uhakika Majisafi ni Desemba 2024
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakazi Dar es Salaam ya Kusini uhakika Majisafi ni Desemba 2024

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya kusini maarufu kama Bangulo na kuahidi kukamilika mapema Desemba 2024 na utahudumia wakazi zaidi ya 450,000 katika kata za Pugu station, Kipinguni, Kiluvya, Kitunda, Mzinga, Kinyerezi na Msigani.

"Siku za nyuma nikiwa Mkuu wa Mkoa maeneo haya ya Bangulo na maeneo jirani yalikuwa na shida kubwa ya maji, nina furaha kuona inakwenda kumalizika kupitia mradi huu, tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk.Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kutoa fedha za mradi mikubwa kama huu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora" ameeleza Lukuvi.

Lukuvi ameongeza kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wake na kumsisitizia Mkandarasi Kampuni ya M/S SINOHYDRO-STECOL JV kukamilisha kazi ili ukamilike kwa wakati na Wananchu waanze mwaka mpya 2025 na huduma ya majisafi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA ambaye ni Mkurugenzi wa mipango na tathmini,Paul Sulley amemuhakikishia Waziri kuwa mradi huo utamalizika kwa wakati katika muda uliopangwa na kunufaisha Wananchi wa Majimbo matatu (3) ya uchaguzi katika Mkoa wa Dar es salaam.

"DAWASA imejidhatiti  katika kukamilisha mradi huu na ifikapo Desemba 2024 ili wananchi  wapate huduma, tumepokea maelekezo  ya kufanya kazi usiku na mchana na tutamuelekeza mkandarasi  kukamilisha kazi kwa wakati" alisema Sulley

Mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya kusini unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 36 na unajumuisha ujenzi wa tenki kubwa la kuhifadhi maji lita Milioni 6 na ulazaji wa bomba kuu la usambazaji maji kwa umbali kilomita 119.