CCM yapinga vikali hoja ya CHADEMA

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:58 AM Oct 10 2024
CCM yajibu hoja ya CHADEMA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejibu hoja iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, kuwa ni dalili kwamba wapinzani wao hao kisiasa wameona watashindwa uchaguzi, hivyo wanatafuta visingizio.

Juzi, Mnyika alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) haijafanya jitihada za kutosha kuelimisha wananchi kuhusiana na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Alisema ni muhimu wananchi wakajitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wakazi kuanzia kesho hadi Oktoba 20 mwaka huu na wameamua kuongeza kasi kwa kuwa wameona suala hilo halijapewa uzito mkubwa wakati ziku za kujiandikisha zinakaribia.

Akijibu hoja hiyo jana, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akiwa ziarani eneo la Malampaka, wilayani Maswa, mkoani Simiyu, alisema hakuna ukweli wowote juu ya hoja za Katibu Mkuu Mnyika kwa kuwa kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika.

Alisema halmashauri zilipewa jukumu la kusimamia uandikishaji huo kwa mujibu wa mwongozo na kanuni za Serikali ya Mitaa.

"Nimeona katika mitandao ya kijamii kiongozi mmoja wa upinzani (bila kumtaja jina), analalamika kuhusu suala hilo kwamba CCM na TAMISEMI kwa makusudi hawahamasishi watu kujiandikisha, hawahamasishi watu kupiga kura. Nikacheka, nikasema 'hawa wenzetu hawa', sisi mikoa yote 18 tunazunguka tunahamasisha, si mnatusikia huko?

"Tunahamasisha watu wajiandikishe, watu wapige kura wanaCCM na wasio wanaCCM kwa sababu tunajua hata wasiokuwa wanaCCM wanaipigia kura CCM kwa sababu ya kazi nzuri ambayo chama chetu kimefanya," alisema.

Katibu Mkuu Nchimbi alisema alisikiliza na kutafakari kauli hiyo na anadhani tayari chama hicho kimeshajua hali ni mbaya; "hakitapata kitu katika uchaguzi huu, hivyo kinaanza kutafuta kisingizio mapema".

"Kama wanavyofanya zile timu kubwa... oooh walitangulia wakaruka ukuta, kwani ukuta ndiyo unaocheza? Watu ndiyo wanaocheza, visingizio waache, twendeni tukatafute kura, wao waombe na sisi tuombe, visingizio hivi ni vya kitoto," alisema Dk. Nchimbi huku akishangiliwa.

Katibu Mkuu huyo pia alipongeza uongozi wa CCM mkoani Simiyu kwa kuendelea kukiunganisha chama, akisisitiza kuwa amehamasika na namna alivyopokewa kwa hamasa kubwa.

"Si kila mwananke anaweza kuwa kiongozi, kama ilivyo kwa wanamume kwamba si kila mwanamume anaweza kuwa kiongozi. Sasa hivi Afrika nzima inatamani kuwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Wengi walidhani hatoweza kuvaa viatu vya Dk. John Magufuli, lakini ameweza na anafanya mambo makubwa.

"Ninyi wenyewe mmeona namna anavyofanya kazi kwa vitendo, miradi mikubwa ya maendeleo inaonekana, shule, huduma za afya ya uzazi kwa kina mama," alisema. 

Aliyekuwa Kada wa CHADEMA na kuhamia CCM, Peter Msigwa alisema kuwa kwa uzoefu wake ndani ya CHADEMA kwa miaka 20, amebaini hawana uwezo wa kuongoza nchi.

Katika ziara hiyo, Balozi Dk. Nchimbi ameambatana na Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Suki), Rabia Hamid Abdalla. 

Ziara hiyo pia imejikita katika kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, kusikiliza kero na changamoto za wananchi kisha kuzitafutia majawabu na kuhamasisha uimara wa CCM kuanzia ngazi ya mashina.