Mtibwa, Songea United hapatoshi

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:46 AM Oct 10 2024
 Mtibwa Sugar
Picha:Mpigapicha Wetu
Mtibwa Sugar

LIGI ya Championship inatarajia kuendelea tena kesho kwa vinara Mtibwa Sugar kuwakaribisha Songea United kutoka Ruvuma katika mchezo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani, Morogoro.

Mtibwa Sugar yenye pointi tisa sawa na Songea United na Stand United ya Shinyanga ndio vinara katika msimamo wa Ligi ya Championship.

Mkuu wa msafara wa Songea United, James Mhagama, aliliambia gazeti hili kikosi chake kiliweka kambi mkoani hapo na kinaendelea vyema na maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo.

Mhagama alisema wachezaji wao wako tayari kupambana na Mtibwa Sugar na wamejiandaa kukutana na mchezo wenye ushindani kwa sababu wanafahamu wapinzani wao wanauzoefu zaidi.

"Tuko hapa (Morogoro), tunaendelea na maandalizi, tutawafuata Mtibwa kule Manungu na huko tunaenda na jambo moja tu la kusaka pointi tatu muhimu, tunajua haitakuwa rahisi kwa kila upande," alisema Mhagama.

Aliongeza malengo ya timu yao ni kupambana na kuhakikisha wanapanda daraja katika msimu ujao ili kuwapa furaha mashabiki wao wa Ruvuma. 

Kiluvya ya Pwani na Transit Camp ambazo hazina pointi hata moja zinaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo.