Magoli 91 yafungwa Ligi Bara, Fountain yang'ara

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:41 AM Oct 10 2024
Magoli 91 yafungwa Ligi  Bara, Fountain yang'ara
Picha:Mtandao
Magoli 91 yafungwa Ligi Bara, Fountain yang'ara

HUKU raundi ya saba ikiwa imeanza, jumla ya mabao 91 yamefungwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, imefahamika.

Kwa mujibu wa takwimu za dawati la Nipashe, mabao hayo yamefungwa katika michezo 50 ambayo imechezwa mpaka sasa wakati ligi hiyo imesimama kupisha michezo ya kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).

Mabao hayo yamefungwa na idadi ya wachezaji 65, huku, straika wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu akiwa kinara, akipachika magoli matano mpaka sasa.

Takwimu zinaonyesha kati ya mabao hayo, 10 yamefungwa kwa penalti na moja la kujifunga.

Waliofunga mabao kwa penalti ni Djuma Shaaban wa Namungo, Heritier Makambo na Shedrack Asiegbu (Tabora United), Jean Ahoua na Leonel Ateba (Simba), Ibrahim Elias (KMC), Salum Kihimbwa (Fountaina Gate), Hassan Dilunga (JKT Tanzania), Nurdin Chona (Prisons) na Stephane Aziz Ki wa Yanga.

Fred Tangalo wa KMC, alijifunga katika harakati za kuokoa katika mchezo ulichezwa Septemba 19, mwaka huu wakati timu yake ikipata kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC, likiwa ni bao pekee la kujifunga tangu kuanza kwa msimu huu.

Katika mabao hayo 91, Fountain Gate ndiyo iliyofunga mengi zaidi mpaka sasa, ikipachika mabao 14, ikifuatiwa na Simba yenye mabao 12, huku Pamba Jiji ikifunga mabao mawili tu ambayo ni machache zaidi kufungwa na timu kwenye ligi mpaka sasa.

Takwimu zinaonyesha katika michezo 50 ya Ligi Kuu iliyochezwa mpaka sasa, 33 imetoa washindi na 17 imemalizika kwa sare.

Pia katika michezo 33 ya ushindi, mechi 19 timu zimeshinda zikicheza viwanja vya nyumbani, na michezo 14 imetoa washindi timu zikicheza ugenini.

Ratiba inaonyesha Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena Oktoba 18, mwaka huu ambapo michezo ya raundi ya nane itaanza, Coastal Union itaikaribisha Dodoma Jiji, JKT Tanzania itakuwa mwenyeji wa Tabora United na Prisons itakuwa nyumbani dhidi ya Azam FC.

Oktoba 19, kutakuwa na patashika nguo kuchanika miamba miwili ya soka nchini, Simba ya Yanga zitavaana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku Oktoba 20, Singida Black Stars itacheza dhidi ya Namungo na Fountain Gate itawaalika KMC.