Zanzibar yapunguza utegemezi wa kuagiza Mbogamboga na matunda

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 03:09 PM Oct 10 2024
Ofisa Kilimo kutoka Taasisi ya Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA) Elisha Mwinyisori, kushoto Akitoa mafunzo kwa mkulima wa mazao ya Mboga mboga na matunda  Ramadhani Omary Juma katika Kijiji cha Umbuji juu ya namna ya matumizi ya Uandaaji wa miche
Picha: Ashton Balaigwa
Ofisa Kilimo kutoka Taasisi ya Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA) Elisha Mwinyisori, kushoto Akitoa mafunzo kwa mkulima wa mazao ya Mboga mboga na matunda Ramadhani Omary Juma katika Kijiji cha Umbuji juu ya namna ya matumizi ya Uandaaji wa miche

HATIMAYE Zanzibar Imeanza kupunguza hali ya utegemezi wa kuagiza mazao ya Mbogamboga na Matunda kutoka asilimia 80 hadi kufikia asilimia 20 kwa Wafanyabishara wa Tanzania Bara,baada kuongeza uzalisha wa mazao hayo kwa kutumia mbinu na teknolojia ya kisasa.

Ongezeko hilo la uzalishaji wa Mbogamboga na Matunda  limekuja baada ya wakulima wa Visiwani humo  kupokea teknolojia za kilimo bora kupitia mradi wa Kukuza kilimo Zanzibar uliokua unatekelezwa  Taasisi ya Kilimo cha Mbogamboga na Matunda (TAHA) pamoja na Taasisi ya Agri Connect.

Wakiongea kwa nyakati tofauti kuhusu  uzalishaji huo  kupitia  mradi wa Kukuza Kilimo Zanzibar (KUZA)  baadhi ya wakulima katika Vijiji vya Mkoa wa Kusini Unguja wamesema tayari  umeleta mabadiliko  makubwa ya kiuchumi katika sekta ya kilimo visiwani humo.

Mmoja wa wakulima hao, Kashinje Mlekwa,kutoka Kijiji cha Umbuji wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja,alisema uzalishaji huo umeongezeka baada kupatiwa mafunzo na  TAHA kuhusu  Mbogamboga na Matunda,na kuondokana na kilimo cha hapo awali ambacho uzalishaji wake ulikuwa duni.

“ Kwenye kilimo  cha awali tulikuwa kama tunasukuma tu hivyo kutokana wengi wao hatukuwa na  elimu na uzalishaji wake ulikuwa ni mdogo sana lakini baada ya kupewa mafunzo ya kilimo bora na TAHA  kila wiki tunatembelewaa na Maafisa wao Ugani  kwaajili utalaam zaidi sasa tumeongeza uzalishaji” alisema Mlekwa.

Mlekwa,amesema baada elimu hiyo ameongeza uzalishaji kwenye kilimo hicho cha Mbogamboga na Matunda kimemuwezesha kuinuka  kiuchumi na  kufanikiwa kujenga Nyumba ya kisasa pamoja na   kusomesha watoto wake kwenye shule mbalimbali.

Naye Selemani Nasoro Selemani,Mkulima ,kutoka Kanda ya Zanzibar,ameshukuru Mradi wa KUZA kwa kuwanganisha na TAHA kwa kuongeza uzalishaji Mbogamboga na Matunda ambao umesaidia sasa kuwa na soko kubwa la mazao hayo Viziwani humo.

Amesema kabla ya mradi huo wa TAHA walikuwa wakilima mazao hayo bila elimu yoyoyote na uzalishaji wake ulikuwa mdogo lakini baada ya kupata elimu ya kilimo cha kisasa uzalishaji wa matunda na mbogamboga umeongezeka na  soko lake limekuwa kubwa na kuuzwa Visiwani humo bila kutegemea kutoka kwa wakulima wa Tanzania bara.

Mariam Issa Hamisi,mwanachama wa Kikundi cha Wakulima Kimbojo kutoka Unguja,amesema kabla ya kuingia kwenye mradi wa TAHA alisema  alikuwa akilima kilimo cha mazoea cha mbogambona ma Matunda kwa kumwaga mbegu chini na kupelekea upotevu wa miche na mingi kukauka na kujikuta wakipata hasara.

“ Baada ya kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa cha Mbogamboga na Matunda ikiwemo kupanda  miche kwenye vitalu na kuchemsha udongo ili kuuwa wadudu na sasa miche haipotei na tunapanda wakati wowote tofauti na kabla ya elimu tulikuwa tunalazimika kupanda jioni na wakati mwingine miche inakufa” amesema Mariam.

Amesema mradi huo umewaongezea uzalishaji wa mboga ikiwemo kwenye kilimo cha Nyanya na Vitunguu  kabla ya alimu hiyo kutoka TAHA alikuwa akipata Tenga 50 kwa msimu lakini hivi sasa anapata tenga zaidi ya 200 kwa msimu mmoja hatua ambayo imemuinua kiuchumi.

Mratibu wa Mradi wa Kukuza Kilimo Zanzibar(KUZA) Carolyne Mlewa,amesema mradi huo umesaidia kupunguza  utegemezi pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani katika mazao ya Mbogamboga na Matunda kwa kujikita na kuangalia uzalishaji pamoja na  upotevu wa mazao shambani ulivyowezwa kutatuliwa.

Amesema  mradi huo wa kilimo cha Mbogamboga na Matunda umewafikia  wakulima 6000  huku wakiondokana na upotevu wa chakula baada ya mavuno kutoka  asilimia 50 na kupungua hadi kufikia asilimia 20 na kuhifadhiwa vizuri bila kuharibika na kuongeza kipato.

Afisa  Maendeleo na  Biashara Alex Allen, amesema pamoja  mradi huo kufikia kikomo lakini umeacha matokea Chanya katika jamii kwa kuyafikia malengo ya mradi wa KUZA uliolenga kukuza  kiuchumi Wanzabari pamoja na kuimarisha lishe ambapo uliweza kuzifikia Shehia 66(Kata) katika Visiwa vya Unguja na Pemba na  kusaidia kuongeza mnyororo wa thamani katika kilimo.

Naye Afisa Kilimo kutoka TAHA,Elisha Mwinyisori,amesema kwa upande wa Zanzibar wanatekeleza mradi wa KUZA kwa kushirikia na Mradi Mkuu wa Agri connect  kwa Ufadhili wa Umoja wa Ulaya ambao ulilenga kuongeza kipato kwenye kaya huku ikifanikiwa kuwabadilisha wakulima kwa kutumia mbinu bora za kilimo cha kisasa kutoka asilimia 30 na sasa wamefikia asilimia 70.