Siku Ya Uoni Duniani; 900 wachunguzwa, 90 wafanyiwa upasuaji

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:09 PM Oct 10 2024
Siku Ya Uoni Duniani; 900 wachunguzwa, 90 wafanyiwa upasuaji
Picha: Mpigapicha Wetu
Siku Ya Uoni Duniani; 900 wachunguzwa, 90 wafanyiwa upasuaji

WATU 900 kutoka maeneo tofauti ya Mkoa wa Pwani na mikoa mingine nchini, wamefanyiwa uchunguzi na matibabu ya macho bure, huku 90 kati yao wakifanyiwa upasuaji.

Matibabu hayo yamefanyika leo katika Kituo cha Afya Chalinze, Wilaya ya Chalinze, mkoani humo, kwa ushirikiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila na Taasisi ya Vision Care ya Korea Kusini.

Bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka MNH-Mloganzila, Dk. Audrey Mwashilemo, amesema kati ya wagonjwa 900 waliofanyiwa uchunguzi na wagonjwa zaidi ya 90 wamefanyiwa upasuaji wa magonjwa mbalimbali ya macho, ikiwamo kutoa mtoto wa jicho.

Miongoni mwa waliofika kupatiwa matibabu hayo ni wananchi kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Mbeya na Dar es Salaam.

Matibabu hayo ni kuadhimisha Siku ya Uoni Duniani ambayo hufanyika Jumatano ya pili ya Oktoba kila mwaka, kauli mbiu mwaka huu  ni: Yapende macho yako, mhamasishe mtoto kupenda macho yake.