Bashungwa:Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:32 PM Oct 10 2024
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa mwenye shati la kitenge akiwa ziarani.
Picha:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa mwenye shati la kitenge akiwa ziarani.

WAZIRI wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema Serikali itaendelea kutenga bajeti kuimarisha miundombinu ya barabara kuwezesha kila eneo kufikika kwa urahisi sambamba na kuvutia watalii na wawekezaji.

Bashungwa ameyasema hayo alipokuwa akikagua barabara ya Nianjema Mjini  Bagamoyo, soko na baadae alipozungumza na wakazi wa mji huo katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kuzindua na kuweka mawe ya msingi.

Amesema mji wa Bagamoyo ni wa kitalii hivyo Serikal itahakikisha inaboresha  barabara  ili ziweze kupitia kwa urahisi na kwamba Km ambazo zimebaki kumjengwa kwa kiwango cha lami zitakamilishwa baada ya michakato kukamilika.

Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara TANROADS Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage kubainisha km za barabara ambazo bado hazijajengwa kwa kiwango cha lami na kuwasilisha katika Wizara ya ujenzi Ili zitengewe bajeti.

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa barabara mita 780 katika mtaa wa Nianjema, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo Mhandisi Bupe Angetile ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hiyo.

Mhandisi Bupe amesema malengo ya Serikali ni kuhakikisha barabara katika mji wa Bagamoyo  zinapitika katika kipindi chote na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii pia kuchochea utalii maeneo ya historia na fukwe za bahati.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo katika mtaa wa Nianjema umekuwa ukifanyika kwa awamu kulingana na fedha zinazotengwa ambazo fedha hizo zinapitika TANROADS na kusimamiwa na TANROADS.