DC Manyara atahadharisha watakaovuruga uchaguzi mdogo

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 06:55 PM Oct 10 2024
Mkuu wa wilaya ya Babati mkoani Manyara Emmanuela Kaganda akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10 ofisini kwake juu ya kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa daftari la wakazi linalotarajiwa kuanza Oktoba 11 mpaka Oktoba 20.
PICHA: JALIWASON JASSON
Mkuu wa wilaya ya Babati mkoani Manyara Emmanuela Kaganda akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 10 ofisini kwake juu ya kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa daftari la wakazi linalotarajiwa kuanza Oktoba 11 mpaka Oktoba 20.

MKUU wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara Emmanuela Kaganda amesema hatarajii kusikia mtu yeyote au kikundi chochote kinavuruga zoezi la uandikishaji wa daftari la wakazi linalotarajiwa kuanza kesho Oktoba 11 mpaka Oktoba 20 katika vijiji, vitongoji na mitaa pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kaganda ametoa onyo hilo leo ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kuanza uandikishaji wa daftari la wakazi na uchaguzi wa serikali za mitaa. 

Mkuu huyo amesema maandalizi ya kuanza kwa zoezi hilo yanaendelea vizuri mpaka jioni kila kitu kitakuwa kiko sawa.

Aidha amesema kwa Halmashauri ya Wilaya ya Babati kutakuwa na vituo 408 vilivyoandaliwa na Halmashauri ya Mji wa Babati kutakuwa na vituo vya kujiandikisha 93.

Pia ameeleza kuwa hata watu walioko gerezani na wagonjwa watafuatwa nyumbani ili wote waweze kushiriki zoezi hili muhimu.

Kuhusu wanafunzi  wa shule za sekondari na vyuo nao amesema watapewa nafasi wajiandikishe.