Robo karne baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, yanayofanya asisahaulike haya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:07 PM Oct 11 2024
 Mwalimu  Nyerere.
Picha:Mtandao
Mwalimu Nyerere.

JUMATATU ijayo, Tanzania itaadhimisha miaka 25 ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano, Julius Kambarage Nyerere, aliyeondoka juu ya uso wa dunia, Oktoba 14, 1999. Ni siku ya kitaifa.

Alifariki dunia nchini Uingereza kwenye Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, ambako alikwenda kwa matibabu ya kansa ya damu.

 Nyerere alipenda zaidi kuitwa Mwalimu, kuliko vyeo vingine vyote alivyokuwa navyo, licha ya kwamba jina lake kuwa kubwa si Afrika tu bali duniani, lakini aliishi maisha ya kawaida kabisa na mwenyewe alipenda kulima kwa kutumia mkono. 

Alikuwa mmoja wa viongozi wanaoheshimika zaidi barani Afrika na kuna wakati alikuwa Mwenyekiti wa Nchi Tano zilizo Mstari wa Mbele Kwenye Ukombozi wa Bara la Afrika. 

Hiyo ilitokana na baadhi ya nchi wakati huo zilikuwa hazijapata uhuru na mwenyewe alisisitiza kuwa, Tanzania haiwezi kuwa huru, kama Afrika yote haitokuwa huru, jambo ambalo limeleta matunda, kwani hadi leo hakuna nchi ambayo haijapata uhuru.

Kwa bahati nzuri alifariki akishuhudia nchi zote zilifanikiwa kuwaondoa wakoloni. Wengi watamweleza kwa makubwa kama hayo aliyoyafanya, Afrika na dunia kwa ujumla, kwani alionekana kama si raia wa Tanzania pekee, bali alitegemewa na nchi nyingi kwa ushauri, busara na maono yake. 

Binafsi nitamwelezea kwa vitu vidogo vya kawaida sana hasa kwenye maisha halisi ya Mtanzania, ambayo ameyafanya kipindi akiwa madarakani.
 Kwanza kabisa, shule zilikuwa bure kabisa, kiasi kwamba hata madaftari, kalamu na vitabu vya masomo vilipatikana shuleni. Mwanafunzi anapomaliza na mwalimu kusaini anakwenda ofisini kupewa kingine.

 Pamoja na ukweli hakukuwapo teknolojia kubwa kama sasa na kuna wakati uchumi wa chini, lakini ni kipindi ambacho wananchi walitibiwa bure kabisa hospitalini.

 Hata chakula kilikuwa kinapatikana bure, hakukuwapo ulazima wa ndugu yoyote kupeleka chakula hospitalini.

 Wagonjwa wa kifua kikuu walilazimika kubaki hospitalini wakiwa wamelazwa mpaka itakapohakikishwa kuwa virusi ya ugonjwa huo vimedhohofika na haviwezi tena kumwambukiza mtu mwingine.

 Kulikuwa na mabomba ya bure, kinamama wakitoka majumbani kwao kwenda kuchota na yakawa maarufu kama mabomba ya bure. 

Cha ajabu mengine yaliwekwa hadi maeneo ambayo hayakuwa na watu wengi kama vile Sinza, Dar es Salaam wakati huo, kukiwa na pori na mashamba ya mpunga.

Kumbe ilishapigwa mahesabu kuwa baada ya miaka 10 na zaidi watakuja kuishi watu, kweli ikawa hivyo. Leo ‘Sinza ni Jiji’ la Dar es Salaam. Palikuwapo malori yanayojulikana kwa sasa kama maboza, yanazunguka mitaani ili wananchi wachote maji. 

Watachota tani zao bila ya malipo hadi waridhike ndipo yanapoondoka. Maeneo ya Gezaulole, Kibugumo, Mwanadilatu, Kunduchi, Bunju, Boko, Kibada watu walipewa maeneo bure, tena kwa kulazimishwa, kipindi cha utawala wake. 

Ilikuwa ni operesheni ya kupunguza watu wasio na kazi na ajira ya kueleweka jijini Dar es Salaam. Walikamatwa na kupelekwa sehemu hizo ambazo wakati huo zilikuwa mapori. 

Wengine walitoroka. Waliobaki, wao wenyewe au vizazi vyao vinakula matunda yake. Ni sehemu ambazo kwa sasa zina huduma zote muhimu, na ardhi imekuwa ghali sana. Hizo zilikuwa ni sera zake.

 Mwacheni tu mzee wa watu alale mahali pema peponi, kwani amefanya mema kwa wananchi wake, ndiyo maana alipofariki wengi walilia sana. Wengine hawakuamini mtu kama Nyerere anaweza kufa mapema kiasi kile, ingawa alishafika umri wa miaka 77.

Huko nyuma awali alishahubiri upeo wa umri wake, kwa kurejea Maandiko Matakatifu kwamba, “Mtu ataishi umri wa makumi mawili matatu na kumi moja... (miaka 70).”