Mwanafunzi aliyepotea siku 26 asimulia alivyoishi akiwa porini

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 12:52 PM Oct 11 2024
Mwanafunzi  Joel Mariki.
Picha: Mtandao
Mwanafunzi Joel Mariki.

MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Bagara, Babati mkoani Manyara, Joel Mariki, amepatikana baada ya kupotea kwa siku 26.

Mariki (14) ambaye alipotea baada ya kuachwa na wanafunzi wenzake walipokuwa Mlima Kwaraa, amesema siku zote hizo alikuwa anaishi kwa kula majani na matunda pori. 

Mwanafunzi huyo alipotea Septemba 14, mwaka huu, akiwa na wenzake kwenye ziara ya kimasomo katika Mlima baada ya kuachwa na kubaki porini.  

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara, Dk. Catherine Magari, jana alithibitisha kumpokea mtoto huyo baada ya kupatikana.  

Dk. Magari alisema hali yake si mbaya lakini wanaendelea kumfanyia uchunguzi. 

Alisema afya yake itaendelea kuimarika akiwa anapatiwa matibabu hospitalini hapo. 

Mama wa mwanafunzi huyo, Germana Wilbard, alikiri kupokea simu ambayo ilikuwa ikimwarifu kupatikana kwa mtoto wake. 

Alisema mtoto wake alipotoka porini, aliibukia kwa mtu na kumweleza kuwa ana njaa ndipo alimpatia uji na akakumbuka namba za simu zake (mama) na kuomba ampigie, alipewa kisha akampigia.  

Alikiri kuwa mtoto wake anaendelea vizuri na anapata matibabu Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara japo amedhoofika. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Makarani Ahmed, akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu, alikiri kuwa ni kweli mtoto huyo amepatikana. 

Ahmed alisema mtoto huyo yuko hospitalini kwa sasa na leo watakwenda kumfanyia mahojiano huko hospitalini. 

"Jitihada za polisi kumtafuta zilikuwa kubwa mpaka tulirusha dron ili kumtafuta,"alisema Ahmed.  

Alisema kwa taarifa ambazo si rasmi, mwanafunzi huyo alijitenga pembeni kwenda kujisaidia na aliporudi  hakuwakuta wenzake, hivyo ameishi porini kwa kula matunda pori akiwatafuta wenzake. 

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Ahmed aliwataka walimu kuchukua tahadhari wanaposafiri na wanafunzi kwa kuwa walivyokuwa wanaulizwa ushahidi wa idadi ya wanafunzi waliokwenda nao Mlima Kwaraa, hawakuwa na majibu ya kuridhisha. 

Pia alisema mtoto huyo alidaiwa kuwa mtukutu, hivyo alisisitiza walimu kutokukubali kubeba wanafunzi wa aina hiyo ili kuepuka usumbufu.