Wataka mbadala adhabu ya kifo

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 11:50 AM Oct 11 2024
Wataka mbadala adhabu ya kifo
Picha: Mtandao
Wataka mbadala adhabu ya kifo

WADAU wa haki jinai wameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka adhabu mbadala kwa kosa la mauaji badala ya kunyongwa hadi kufa kwa kuwa haijawahi kutekelezwa tangu serikali ya awamu ya tatu huku wafungwa wengi wakikaa magerezani wakizidi kuumia kisaikolojia.

Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani yenye kaulimbuiu ‘Adhabu ya Kifo Hailindi Mtu Yeyote: Iondolewe Sasa’, walisema wafungwa hao ni mzigo kwa serikali kutokana na kutunzwa kwa fedha za Watanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alisema lengo la adhabu ni kurekebisha tabia ili mtu awe mfano kwa wengine lakini wengi wako gerezani kwa muda mrefu na hawajui hatima yao.

“Adhabu ya kifo haifanyi kazi yoyote kwa kuwa wanalishwa kwa gharama za serikali, hivyo ni mzigo kwa taifa, Adhabu hii haijawahi kutekelezwa mwaka 1994. Ni  miaka 30 sasa. Kama  imeshindikana kutekelezwa ni muhimu kukawa na mbadala,” alisema.

Pia alisema hakuna ushahidi kwamba adhabu hiyo imepunguza uhalifu bali kumekuwa na makosa mengi na kwamba hivi karibuni nchini  Iran, kuna adhabu ya kifo na hata mwizi wa simu anapata adhabu hiyo na kwamba wamenyonga zaidi ya 200 lakini bado matukio yapo.

Dk. Henga alisema wako waliohukumiwa kifo kimakosa na baada ya muda wanaachiwa baada ya kukata rufani huku wengine hawajui taratibu ili wapate msaada kisheria na kwamba mtu anaponyongwa hakuna namna yoyote inawezekana kumrejesha.

“Tanzania ni nchi ya demokrasia lakini kutokana na mizizi ya kikoloni ndiyo maana sheria hiyo imeendelea kuwapo. Kuna mikataba mingi tumeridhia ukiwamo Mkataba wa Haki za Binadamu na Kiraia ambao unatambua haki za kuiishi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Women Aid and Criminal Justice (WACT), Elizabeth Majagi, alisema wanawake wengi waliowatembelea wenye umri wa miaka 18 wanasema wengi walidanganywa wakubali makosa kisha watasaidiwa kutoka mbele ya safari.

“Watu wanasota sana gerezani hata kesi haijasikilizwa kwa miaka mingi na hawafahamu hatima yao. Segerea wako watatu wamekaa miaka tisa, mmoja  aliingia akiwa na miaka 19. Hawajui  kesi zao na uelewa wa sheria ni mdogo na wanaotoa msaada wa sheria ni wachache,” alisema.

Alisema Kampeni ya Msaada wa Kisheria na Mama Samia imefika kwenye magereza mengi na kutoa msaada kwa wafungwa wengi wenye uelewa mdogo kisheria na kwamba wafungwa wengi hawawezi kukata rufani na wanatumikia kifungo pasipo utekelezaji.

Mkurugenzi wa Tanzania Ex-prisoners Foundation (TEPF), Rose Male, alisema alishtakiwa kwa mauaji ya dereva wa bodaboda ambaye alimpigia simu kutumia usafiri wake halafu baadaye aliuawa. Kutokana na tuhuma hizo, alisota mahabusu kwa miaka minne na baadaye kuhukumiwa kifungo cha kunyongwa hadi kufa lakini alitumikia miaka miwili kisha akakata rufani.

“Wengi ni wazee kutokana na kukaa kwa muda mrefu kutokana na adhabu ya kifo kutotekelezwa. Wengi wanaishi kwa hofu kwa kuwa wanahisi watanyongwa wakati wowote, mlango ukifunguliwa mtu anawaza nimekuja kuchukuliwa kwa ajili ya kunyongwa,” alisema.

Alisema mfungwa wa adhabu ya kifo haruhusiwi kutembelewa bila ruhusa ya mkuu wa wilaya na wengi hawajui huo utaratibu ili wamfikie ndugu yake jambo ambalo linawanyima haki ya kupata taarifa.

“Katika kazi hizi nilikutana na dada mmoja alihukumiwa mwaka 1999 lakini hajawahi kupata nakala ya hukumu yake na hana rekodi yoyote ya kesi yake hata hakumbuki mahakama aliyohukumiwa, jambo ambalo limemnyima haki ya msaada wa kisheria,” alibainisha.

Male alisema mtu ana kesi ya mauaji anapewa wakili wa serikali ambaye wakati mwingine hafanyi kwa ubora kwa kuwa wanawaambiwa washtakiwa wakiri makosa  kwa kuwa watatoka mbele ya safari.

Alisema wafungwa wanapokuwa gerezani huzalisha lakini wanapomaliza vifungo hupewa nauli tu, huku wengine wanaporudi wanakuta familia zimeparaganyika, hivyo  hawana pa kuanzia.

“Tumefanya utafiti tumebaini asilimia 60 ya walioko gerezani ni wakosaji wa kujirudia. Maana yake mtu anakwenda uraiani anapokewa kwa unyanyapaa, mali zake zimepotea, familia imeparaganyika hana pa kuanzia. Kama wanazalisha wakiwa gerezani basi serikali iwe inawawekea kwenye akaunti zao fedha kidogo ili wanapomaliza kifungo wawe na kianzio cha maisha,” alisema.

Mwakilishi wa Children Education Society Organization (CHESO), Utty Mwang’amba, alisema kuna unyanyapaa kwenye jamii kiasi cha wanaotoka gerezani kushindwa kuoa au kuolewa na wengine kupata matatizo ya afya ya akili.

“Leo kuna familia imenitafuta inasema inahama eneo wanaloishi kutokana na unyanyapaa wanaokutana nao. Wanaonyoshewa  vidole sana, wanaambiwa usiolewe pale, usioe pale. Mwingine anatoka gerezani anakuta mwenza wake ameshaoa au kuolewa, hivyo  anakosa pa kuishi. Lazima  tuwaangalie hawa watu,” alisema.

Kuhusu sababu za mauaji, wachangiaji hao walisema wengi walioko gerezani ni kwa sababu ya kulipiza kisasi, wivu wa kimapenzi, imani za kishirikiana kutaka kupata utajiri na msongo wa mawazo.

SERIKALI YAJIBU 

Mwakilishi wa Wizara ya Katiba na Sheria, Wakili Emmanuel Mbega, alisema suala la mabadiliko ya sheria ni mchakato na kwamba serikali inaendelea kupokea maoni ya wananchi na  ili sheria ibadilishwe lazima kuwe na utafiti wa kina.

Alisema ni wajibu wa wakili kutoa msaada wa kisheria na kwamba malalamiko ya kwanza wanawalazimisha watuhumiwa kukiri makosa watalifuatilia, ili watekeleze majukumu yao kwa mujibu wa sheria.