Askofu Malasusa atoa somo uchaguzi S/Mitaa

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:22 PM Oct 11 2024
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.
Picha:Mtandao
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, amewapa somo wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu, akiwataka wasijisahaulishe kwamba matendo yao yanapaswa kuwa yamenyooka kuanzia duniani hadi mbinguni.

Malasusa, alisema kuna idadi kubwa ya watu hawatambulishiki kwenye jamii hivi sasa, kwa sababu ya matendo yao, hata wake zao hawawezi kuwatambulisha.

Alikuwa akihubiri jana katika Usharika wa Uuwo-Mwika wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT, wakati wa ibada ya maziko ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC, Prof. John Shao (80).

Prof. Shao, alifariki dunia Oktoba 6, mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufani ya KCMC.

"Kuna watu hawatambulishiki kwenye jamii kwa sababu ya matendo yao, hata wake zao hawawezi kuwatambulisha. Profesa Shao yeye alikuwa anatambulishika wakati wa uhai wake. 

"Tunaenda kwenye uchaguzi na wagombea watajitangaza sana mambo yao, wasisahau wanatakiwa mambo yao yanyooke na wajitangaze mbinguni."

Katika maziko hayo, viongozi wengine walioongozana na Askofu Dk. Malasusa, ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Frederick Shoo na Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenberg Mdegela.

Akisoma wasifu wa hayati Prof. Shao, mtoto wa marehemu, Kunda Shao, alisema baba yake (Prof. Shao), aligomea matibabu ya nje ya nchi, akiamini madaktari wa ndani yaani Tanzania wana uwezo wa kufanya matibabu hayo.

Alisema baba yake, alikuwa akiugua ugonjwa wa saratani ya tezi dume.

Mwakilishi wa Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara hiyo (MoH), Dk. Saitore Laizer, alisema serikali haitasahau mchango wa nguli huyo katika mifumo ya sekta ya afya nchini.

"Kanisa limepata pigo, lakini pia sekta ya afya katika eneo la tiba na mafunzo, tumepata pigo. Profesa Shao alikuwa ni mbuyu mkubwa, lakini ulikuwa unazaa matunda kila mwaka. Serikali na sekta ya afya, haitasahau mchango wake hasa eneo la microbiolojia na immuniolojia," alisema Dk. Saitore.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufani ya KCMC, Prof. Gilleard Masenga, alisema katika kuuenzi mchango wa Prof. Shao, Shirika la Msamaria Mwema (GSF), limepanga kulipa hadhi ya jina lake moja ya majengo ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba cha Tumaini (KCMCo).

Taarifa ya kifo chake, ilitangazwa na Katibu Mtendaji wa Shirika la Msamaria Mwema (GSF) na Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Prof. Gilleard Masenga.

Wakati wa uhai wake, Prof. Shao, aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa GSF, Makamu Mkuu wa Kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (TUMA).

Prof. Shao, alizaliwa mwaka 1944, alisomea shahada ya magonjwa ya vimelea mbalimbali pia amewahi kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1978-1981, Mshauri wa wanafunzi UDSM, kuanzia 1981-1986, Profesa Mshiriki mwaka 1982-1990, na Profesa tangu 1986. 

Tangu mwaka 1994 alikuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Umoja wa Madaktari Afrika na mwaka 1992, aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Sekta ya Afya Tanzania, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Mwaka 1990-1992.

Katika maisha yake ya kitaaluma, aliandika na kuchapisha machapisho 150 ya kitaifa na kimataifa na alikuwa na maono binafsi kama kuanzisha KCRI na KCMCO.