Mkurugenzi PSSSF awatembelea wapangaji, kilele Wiki ya Huduma kwa Wateja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:48 PM Oct 11 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Abdul-Razaq Badru,  akimkabidhi zawadi Balozi Mdogo wa Korea hapa nchini, Lee Seungyun.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Abdul-Razaq Badru, akimkabidhi zawadi Balozi Mdogo wa Korea hapa nchini, Lee Seungyun.

WAKATI ya Wiki ya Huduma kwa Wateja inafikia kilele leo Oktoba 11, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Abdul-Razaq Badru, amewatembelea wapangaji wa jengo la Golden Jubilee Towers jijini Dar es Salaam, moja ta vitega uchumi vya mfuko huo, kwa nia ya kuwashukuru na kusikiliza changamoto zao.

Miongoni mwa wapangaji wakubwa kwenye jengo hilo ambao amewatembelea ni pamoja na Ubalozi wa Korea nchini na Kampuni ya TMRC.

Akizungumza na Balozi Mdogo wa Korea hapa nchini, Lee Seungyun, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, ameushukuru Ubalozi wa Korea kwa kuendelea kuwa wapangaji waaminifu kwenye jengo hilo na kumkaribisha kwenye majengo mengine ya vitegauchumi kwa ajili ya kupangisha kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo makao makuu Dodoma.

Naye balozi huyo mdogo wa Korea, amemshukuru Badru kwa kuwatembelea na kumuahidi kuwajulisha wadau wengine kuhusu nafasi hizo za kupanga.

Aidha, Badru amemshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya, kwa kuendelea kuwa mpangaji mwaminifu katika jengo hilo.

“Katika maisha ya kawaida, katika biashara tunategemeana, mmoja akipungua umuhimu unaondoka, wiki hii ni wiki ya kutafakari, ni namna gani tunaweza kufanya vizuri, namna gani tunaweza kufanya tofauti au panapokuwa na haja ya kufanya marekebisho tuna harakisha kwa kiasi gani.” amesema.

Tunawapongeza sana na tunawaahidi utayari wetu wa kutoa huduma zilizobora na kushirikiana panapotokea changamoto.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya, yeye amepongeza hatua ya Mkurugenzi Mkuu Badru, kuwatembelea kwani ni heshima kubwa kwao na wamejiona kuwa wanathaminiwa na mfuko.

“Tunachoiweza kuahidi ni kuendelea kuwa wapangaji waaminifu kwenye jengo hili na hata tunapofikiria kuongeza zaidi shughuli zetu tunaona hapa tuko mahala pazuri zaidi.” amesema Mgaya

Halikadhalika Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji PSSSF, Fortunatus Magambo yeye ameitembelea benki ya CRDB ambao ni wapangaji wa muda mrefu kwenye jengo la kitegauchumi la PSSSF, Garden Avenue Towers, zamani PPF Tower wakiwa hapo toka mwaka 2000.