RC Mtwara awataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha

By Baraka Jamali , Nipashe
Published at 05:15 PM Oct 11 2024
RC Mtwara awataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
Picha:Bakari Jamali
RC Mtwara awataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amezindua rasmi zoezi la kujiandikisha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika mtaa wa Shangani East, utakaofanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Kanali Sawala amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu kwa maendeleo ya demokrasia nchini.

Kanali Sawala ameeleza kuridhishwa kwake na mwitikio wa awali wa wananchi waliojitokeza, akitoa wito kwa viongozi wa mitaa na vijiji kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kujiandikisha. “Leo nimeungana na wananchi kujiandikisha na ninaendelea kuwasihi wote kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha haki zao za kidemokrasia zinalindwa,” amesema Kanali Sawala.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewahimiza wananchi kutumia muda uliopo kujiandikisha mapema ili kuepuka msongamano siku za mwisho za zoezi hilo. “Ni muhimu kila mmoja wetu ajiandikishe mapema ili kuepusha changamoto za dakika za mwisho,” amesema Mwaipaya.

Vijana kutoka vyuo vikuu na vyuo vya kati walijitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi hilo. Juma Omari, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Stella Maris, ametoa wito kwa vijana wenzake kushiriki kwa wingi, akisisitiza kuwa kushiriki uchaguzi ni haki yao ya kikatiba. “Kama vijana, ni muhimu tujue kuwa huu ni wajibu wetu kama raia wa nchi hii,” amesema Omari.

1

Hawa Saidi Sule, mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu, amewahamasisha vijana wa kike kujiandikisha na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. “Ninawahimiza wasichana wenzangu, tujitokeze kujiandikisha na kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa uchaguzi,” amesema Hawa.

Zamda Jafari, Mkazi wa Shangani West, ameeleza kuwa wanawake wamekuwa wakijitokeza kwa idadi ndogo, akiwasihi kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu. “Tunahitaji wanawake wengi zaidi kwenye siasa ili kuhakikisha tunapata nafasi katika ngazi za uongozi,” amesema.

Inakadiriwa kuwa takriban asilimia 60 ya vijana wa Manispaa ya Mtwara Mikindani tayari wamejiandikisha, lakini bado juhudi za ziada zinahitajika kuwafikia wale ambao hawajajiandikisha. Viongozi wa mitaa wametakiwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuhakikisha wanatambua umuhimu wa zoezi hilo.

Katika tamko lake, Waziri Mchengwela alisema, "Uchaguzi wa serikali za mitaa ni nguzo muhimu ya demokrasia nchini mwetu. Tunahitaji ushiriki wa kila mwananchi ili kuhakikisha sauti zetu zinaskika na haki zinalindwa."

Zoezi hili la kujiandikisha ni fursa ya pekee kwa wananchi kuweza kuchagua viongozi wanaowawakilisha katika ngazi za mitaa na vijiji, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha amehakiki taarifa zake na amejiandikisha.