WAJIKI yazindua kampeni kupambana na rushwa ya ngono

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:20 PM Oct 11 2024
Mkurugenzi wa WAJIKI wa kwanza kulia akiwa na viongozi wanzake siku ya uzinduzi wa kampeni hiyo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa WAJIKI wa kwanza kulia akiwa na viongozi wanzake siku ya uzinduzi wa kampeni hiyo.

KATIKA kupambana na rushwa ya ngono kwa wasichana na wanafunzi Taasisi Isiyo ya Kiserikali, ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJIKI), imezindua kampeni ya kutoa elimu kwa jamii na madereva ili kukomesha vitendo hivyo.

Uzinduzi wa kampeni hiyo yenye kauli mbiu isemayo 'vunja ukimya, safari salama bila rushwa ya ngono inawezekana' umefanyika leo Bunju A Wilayani Kinondoni mkoa wa Dar es salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurungezi wa taasisi hiyo Janeth Mawinza, amesema kusudio la kampeni hiyo ni kutoa elimu ya ulinzi kwa wanafunzi shuleni na kupinga vita rushwa ya ngono kwa madereva wa daladala, bajaji na bodaboda.

Amesema pia kampeni hiyo itajikita katika  kuwashawishi wanawake kushiriki kugombea nafasi za uwongozi wa serikali za mitaa na hata uwongozi wa juu, ili kufikia lengo la hamsini kwa hamsini.

“Tunaamini kampeni hii italeta matokeo chanya katika vitu vitatu ambavyo tumelenga katika kutoa elimu kwa madereva ambao moja kwa moja ndio wanawabeba wanafunzi na wasichana kuwatoa sehemu moja kwenda nyingine, pia kuwapa ushawishi wanawake kugombea uongozi na kutoa elimu ya ulinzi wa wasichana mashuleni.” amesema Janeth 

Akizungumza namna kampeni hiyo, ilivyoleta matokeo chanya katika Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni alisema baada ya madereva hao kupatiwa elimu hiyo, wameona mwitikio na mabadiliko makubwa dhidi ya ukatili wa kingono kwa wanafunzi.

Vile vile amesema kuwa wanahitaji kuwafikia wanafunzi wasiopungua 35,000 katika shule 6 ndani ya kata ya Bunju A, shule za msingi 4 na sekondari 2, na kutoa elimu kwa bodaboda wasio pungua 200 na walimu wasiopungua 100.

Ofisa wa tathmini na ufuatiliaji kutoka katika taasisi hiyo, Hancy Obote, amesema maafisa ustawi wajamii watasaidia kufahamu watoto wanaokutana na changamoto ya ukatili wa kingono katika kata hiyo, kutokana na kazi yao inaendana na kampeni hiyo.

“Maafisa ustawi wa jamii na mafisa maendeleo ndio serikali yenyewe, hivyo tunaamini kuwa kampeni hii itakuwa endelevu hata ikatokea muda wetu umekwisha  basi watakuwa tayari kuelea na kampeni hii ya vunja ukimya, safari salama bila rushwa ya ngono ili kutokomeza ukatili huu.” Amesema  Obote

Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Bunju, Lilian Chillo, alimpongeza Janeth kwa kuanzisha kampeni hiyo na kwamba wameipokea kwa mtazamo chanya wakiamini itaenda kuleta mabadiliko. 

Pia amesema wapo tayari kushirikiana na Taasisi yake ambayo pia inafadhiliwa na Womeni Fund Tanzania Trust (WFT-T) katika kuhamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uwongozi serikalini, hivyo wanaamini kuwa kampeni hiyo itawawezesha wanawake wa Kata ya Bunju kujitokeza.

“Nimefurahi kusikia kwamba kampeni hii sio kwamba imekuja kuanzia hapa Bunju A, imeshawafikia na kuwasaidia wasichana, wanafunzi wengi katika Mkoa wetu, kwamba mlianza kwenye Kata nyinginezo ambazo nimezisikia hapa na kuwa mmeona kuwa ni kwa namna gani watoto wetu wapo hatarini, hivyo tunapaswa kuwasaidia kwa njia hii.”amesema Lilian