RC Malima, aonya watakaovuruga zoezi la uandikishaji

By Ashton Balaigwa , Nipashe
Published at 06:30 PM Oct 11 2024
Mwandikishaji wa Daftari la kupiga kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kituo cha LITA Manispaa ya Morogoro,Aisha Muwinge (kushoto) aliyekaa,akimwandikisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adam Malima(kulia) ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa uandikishwaji.
Picha: Ashton Balaigwa,Morogoro.
Mwandikishaji wa Daftari la kupiga kura la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kituo cha LITA Manispaa ya Morogoro,Aisha Muwinge (kushoto) aliyekaa,akimwandikisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adam Malima(kulia) ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa uandikishwaji.

MKUU wa Mkoa wa Morogoro,Adam Malima ameonya Viongozi wa Vyama wa Vyama vya Siasa,Makundi ya Watu na Viongozi wa Kijamii wenye nia ovu ya kushawishi au kuharibu zoezi la uandikishaji katika Daftari la wapiga kura kwaajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa wasithubuti kufanya hivyo kwani hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

Malima ametoa onyo hilo,ikiwa wakati akizungumza na Waandishi wa Habari,mkoani Morogoro mara baada ya kuzindua zoezi hilo la uandikishaji kwa mkoa huo katika Kituo cha Chuo cha Mifugo cha LITA kilichopo Kata Manispaa ya Morogoro.

Amesema hakuna Kiongozi wa Chama chochote  au mtu yoyote mwenye mwenye Mamlaka ya kumzuia mtu yoyote mwenye sifa ikiwemo ya umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kumzuia kujiandikisha kwenye zoezi hilo kwakuwa ana haki ya kushiriki na  kuchagua kiongozi anayemtaka kwenye uchaguzi huo wa Serikali za mitaa.

“Nasisitiza hasitokee kiongozi yoyote awe wa Kisiasa ,Kijamii,Dini au mtu yoyote kumzuia au nia ovu ya kukwamisha zoezi hili la uandikishaji kwenye Daftari kwaajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa  liloanza leo Octoba 11,2024,huyo tutamchukulia hatua kali sana “ amesema Malima.

Malima amesema viongozi hao hasa wa vyama vya uchaguzi vishiriki kuhakikihsa vinahamasisha wananchi wanajitokeza kujiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wenye sifa na wanaowataka kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro,amesema mkoa umejipanga kuandikisha watu wenye sifa ya kuandikishwa 1.816,485 sawa na asilimia 53.2 ya watu 3,414.507 wanaokadiriwa kuwepo mkoani humo kwa mwaka 2024 kulingana na ongezeko la asilimia 3.4 kutokana na Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambayo ni 3,197,104.

Hili naliweka wazi na kila mtu alielewe,katika zoezi hili la uandikishwaji kwenye Daftari la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,sitarajii kuona mtu mwnye akili timamu kuhamasisha watu wasijiandikishe ili kuchagua viongozi wanaowataka kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano” alisema Malima.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Morogoro,alisema katika zoezi hilo jumla ya vituo 3752 vitatumika kuandikisha wapiga kura huku vikiwa na jumla ya waandikishaji 3998 wapo kwenye vituo vyote vilivyopangwa.

Akielezea zoezi hilo la uandikishwaji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro,ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Emmanuel Mkongo,amesema limeanza vizuri na vituo vyote vimefunguliwa mapema na muitikio wa wananchi ni mkubwa.

Amesema katika Kituo cha LITA muitikio umekuwa mkubwa kwani kwa kituo hicho kinategemewa kuandikisha wananchi 506 lakini kutokana na idadi ya watu waliojitokeza kwa siku moja ya zaidia ya watu 200 kuna uwezekano wa zoezi hilo kwa kituo hicho likachukua siku tano kati ya siku 10 zilizowekwa.

Mkurugenzi huyo wa Manispaa amesema malengo ni kuandikisha jumla ya wananchi 283,836 na vipo vituo kwenye Kata ya Lukobe na Mkundi kuna kituo kimoja kina idadi ya watu zaidi ya 5000 lakini wameweka mikakati badala ya kuwa na mwandikishaji mmoja wameweka wawili na watakuwa wakiangalia hali inavyoongezeka wanaongeza idadi ya waandikishaji.

 Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba,amesema wanatarajia kuandikisha watu 120,000 na tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha wanafikia malengo yao ya uandikishaji katika halmashauri hiyo.

Ametaja mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa watu wenye mahitaji maalumu na wananchi wa kawaida kwa kufanya Matamasha kwa kila Tarafa zilizopo katika wilaya hiyo yatakayofanyika Octoba 14,2024  siku ya mapunziko ya Kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Mkoa wa Morogoro,Jacob Kayange,alisema vifaa vyote vimefika kwa wakati katika vituo vyote vilivyopo kwenye mitaa na vitongoji na hakuna changamoto yoyote iliyojitokeza ya kukwamisha zoezi hilo.