Wakazi milioni 1.2 wanatarajiwa kujiandikisha Pwani, Kunenge awaita wananchi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 09:43 PM Oct 11 2024
Wakazi milioni 1.2 wanatarajiwa kujiandikisha Pwani, Kunenge awaita wananchi
Picha: Julieth Mkireri
Wakazi milioni 1.2 wanatarajiwa kujiandikisha Pwani, Kunenge awaita wananchi

Zaidi ya wakazi milioni 1.2 wa Mkoa wa Pwani wanatarajiwa kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, uandikishaji ambao umeanza leo Oktoba 11,2024 hadi Oktoba 20.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amezindua rasmi zoezi hilo katika Mtaa wa mkoani, Kata ya Tumbi, Halmashauri ya Mji wa Kibaha.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kujiandikisha, Kunenge ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kutumia haki yao ya kuchagua viongozi wanaowataka kwenye ngazi za vijiji na mitaa.


 Amesisitiza kuwa maendeleo yanaanzia ngazi za chini, na uchaguzi huu ni muhimu kwa nafasi hizo kabla ya uchaguzi mkuu ujao. "Wananchi mnatakiwa kutumia nafasi yenu kujiandikisha ili muweze kuchagua viongozi mnaowataka, watakaowasemea matatizo yenu," amesema Kunenge.


Mkoa wa Pwani umetenga vituo 2,374 vya kujiandikishia, lengo likiwa ni kupunguza msongamano na kurahisisha upatikanaji wa huduma.


 Emmanuel Masele, mmoja wa wananchi waliojitokeza kujiandikisha, amewataka wananchi wengine kujitokeza kwa wingi ili kuchagua viongozi wanaowataka na kuepuka malalamiko ya baadaye.


Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Pwani una wakazi 2,024,949, wakiwemo wanawake 990,616 na wanaume 1,026,331, huku ukiwa na vijiji 417, mitaa 73, na vitongoji 2,028.