Adaiwa kuua mke kisa nyama ya mbuzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:34 PM Oct 11 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Shadrack Masija.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Shadrack Masija.

JESHI la Polisi mkoani Rukwa linamshikilia mwanamume (jina limehifadhiwa) mkazi wa mtaa wa Chitepo, Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga, kwa tuhuma za kumpiga kisha kumkata na kisu mke wake, Hawa Suleiman (31) na kumsababishia kifo.

Chanzo cha mauaji  hayo kinadaiwa ni wivu wa kimapenzi. Inadaiwa kuwa mume huyo alichukizwa na kitendo cha kukuta mke wake amepika nyama ya mbuzi wakati hakumwachia hela yoyote ya matumizi. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Shadrack Masija, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi mjini Sumbawanga na anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote upelelezi wa awali utakapokamilika. 

SACP Masija alisema Hawa alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hiospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruswa mjini hapa. 

 Kwa mujibu wa Kamanda Masija, tukio hilo lilitokea Oktoba 9, mwaka huu, majira ya saa 7:00 baada ya kuzuka ugomvi baina ya wanandoa hao ndipo mwanamume alipoanza kumpiga mke wake kwa kutumia kipande cha mti na kumkatakata sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia kisu. 

Mmoja wa majirani wa wanandoa hao, Editha Kawia, kabla ya mauaji hayo, mtuhumiwa aliondoka nyumbani kwake na kumwacha mke wake na kwenda kwenye shughuli zake bila kumwachia hela yoyote ya matumizi.

 Alisema majira ya mchana, mwanamume huyo alirejea nyumbani na kukuta mke wake amepika nyama ya mbuzi na alipomhoji alikopata fedha  ya kununua nyama hiyo,  hakutoa majibu yaliyomridhisha.

 ''Mtuhumiwa alichukua sufuria iliyokuwa na  mboga hiyo na kwenda kumwaga nje ndipo alipotoa Sh. 2,500 na kumpa mke wake ili akanunue mboga nyingine ambayo wataitumia kama kitoweo kwa siku hiyo kisha akaondoka zake,” alisema. 

Kwa mujibu wa jirani huyo, baada ya muda, mwanamume huyo alirejea nyumbani akakuta mke wake amenunua dagaa na kupika hali iliyomkera na kudai kuwa hawezi kula dagaa na kutishia kumpiga. Ili kujiepusha na kipigo, alisema mwanamke huyo alikimbia na kuondoka nyumbani.

 “Hawa alikaa huko alikokimbilia na akarudi nyumbani majira ya saa 6;30 usiku akamkuta mume wake nyumbani. Alipoingia  ndani ndipo ugomvi ulipoanza na mwanamume huyo akaanza kumpiga mke wake akimtuhumu kuwa na tabia mbaya.

 “Baada ya kumpiga muda mrefu jirani yake alikwenda kuwagongea ili awasuluhishe lakini mwanamume alimjia juu jirani huyo akidai kuwa hayamhusu na anaweza kumpiga hata pia, kauli iliyomsababishia hofu na kuamua kurudi ndani ya nyumba yake,” alisema.

 Jirani huyo alibainisha kuwa mwanamume aliendelea kumpiga Hawa kwa muda mrefu kisha akaacha. Alisema kulipokucha alikwenda kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa ndipo walipofika nyumbani kwa mtuhumiwa, wakamchukua akiwa na majeraha na kumpeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu.