Taarifa miradi yenye dosari mbio za Mwenge kukabidhiwa kwa Rais

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 12:28 PM Oct 11 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mtandao
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amesema taarifa ya miradi iliyobainika kuwa na dosari katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, itakabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua zaidi.

Pia amesema katika maadhimisho ya wiki ya vijana kwa mwaka huu kutakuwa na makongamano kwa ajili ya vijana yanayolenga masuala mbalimbali ikiwamo elimu ya sera mpya ya maendeleo ya vijana toleo la 2024 na mafanikio ya miaka 60 ya Mwenge wa Uhuru.

Akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo, kilele cha mbio hizo sambamba na kumbukumbu ya miaka 25 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yatakayofanyika jijini Mwanza, Waziri Kikwete alisema kupitia mbio hizo, kumebainika kuwapo na dosari katika baadhi ya miradi ikiwamo kujengwa chini ya kiwango na kutokuwa na usimamizi mzuri.

“Taarifa ya miradi iliyotembelewa na Mwenge nitakabidhiwa kwa Rais Samia, siku ya kilele kwa hatua zaidi,” alisema.

Alisema kwa mwaka huu elimu ya mbio hizo itatolewa ili kusaidia kuongeza uelewa kwa Watanzania ambao wanahisi kuziendeleza ni upotevu wa fedha.

“Kuna watu wanaona Mwenge huu ni kama tochi, kuna wengine wanatamani usiwapo. Tunataka kueleza kwa nini Mwenge wa Uhuru upo. Usiache mambo yakazungumzwa, inawezekana kuna watu hawajui umuhimu, hii ni kama wanavyosherehekea siku zao za kuzaliwa,” alisema.

Kuhusu Wiki ya Vijana, Kikwete alisema itazinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, leo na inalenga kuwakutanisha vijana kujadili fursa na vikwazo vinavyowakabili katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema vijana watajengewa uwezo katika uongozi na kuhamasishwa kujitambua na kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali.

Ridhiwani alisema hadi sasa serikali imewezesha vikundi vya vijana zaidi ya Sh. bilioni 31.

“Tunatarajia zaidi ya vijana 500 watafanya maandamano ya amani wakiwa wamebeba ujumbe mbalimbali na sisi serikali tutakuwapo kuchukua na kufanyia kazi,” alisema.

Kuhusu Kumbukizi ya Miaka 25 ya Mwalimu Nyerere, alisema, ibada maalum ya kumuenzi itafanyika katika Kanisa Katoliki Nyakahoja, mkoani Mwanza.