Waziri Kombo ahimiza ushirikiano wa kibiashara

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 12:46 PM Oct 11 2024
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Picha: Mtandao
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.

TANZANIA imesisitiza umuhimu wa kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi marafiki, ikiamini kuwa hiyo ndiyo njia bora zaidi ya kukuza uchumi kwa manufaa ya wananchi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema hayo jana Helsinki, Finland, aliposhiriki kikao cha Mashauriano ya Kisiasa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland, Elina Valtonen na Naibu Mawaziri wa Wizara hiyo, Pasi Hellman anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Kimataifa na Jarno Syrjälä anayeshughulikia biashara za kimataifa.

Kombo alisema Tanzania imefanya mabadiliko makubwa ya mifumo ya sera na sheria ili kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuvutia uwekezaji.

Kupitia hali hiyo, alitoa wito kwa wawekezaji wenye mitaji na dhamira ya dhati ya kuwekeza, waondoe hofu kuhusu Tanzania kwa kuwa ni mahali salama kwa wawekezaji na mitaji yao.

Waziri Kombo aliishukuru serikali ya Finland kwa kufanya juhudi kubwa ya kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali kama vile misitu, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), mifumo ya ulipaji kodi, hali ya hewa na elimu. 

Alisema juhudi hizo zimechangia kuifikisha Tanzania ilipo sasa na kuwaomba mawaziri hao waendeleze juhudi hizo huku wakihimiza kampuni za nchi yao  kuwekeza Tanzania ambayo ina fursa nyingi ambazo hazijatumiwa kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo mitaji midogo na teknolojia duni.  

Balozi Kombo aliainisha maeneo ambayo Finland inapaswa kuwapa kipaumbele katika ushirikiano wake na Tanzania kuwa  ni pamoja na uhawilishaji wa teknolojia,  nishati, viwanda vya kuongoza thamani, elimu ya ufundi, masuala ya kijinsia na haki za wanawake na masuala ya kidijiti.

Alisema maeneo hayo yakifanyiwa kazi ipasavyo, yataongeza nafasi za kazi na ni suluhisho la moja kwa moja la tatizo la ajira nchini.

Kombo aliongeza ni wakati mwafaka wa nchi ya Finland kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania katika fani ambazo nchi hiyo pia inazihitaji kwa kiasi kikubwa. 

Alisema Tanzania iko tayari kutuma vijana ambao watasomeshwa kwa viwango vinavyohitajika katika fani hizo ili kuziba pengo kama vile la wataalamu wa afya hasa wauguzi katika nchi za Ulaya.

Viongozi hao pia walijadili suala la amani na usalama duniani na kusisitiza umuhimu wa kutatua migogoro inayoendelea kwa njia za kidiplomasia.

Waziri Kombo aliwahakikishia viongozi hao kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika suala la kulinda amani na kwamba hivi sasa, Rais Samia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema kuna sababu mbalimbali zinazosababisha migogoro barani Afrika ikiwa ni pamoja na uwepo wa vijana wengi wasio kuwa na ajira. Alisema nchi zilizoendelea hazina budi kusaidia programu za kuongeza ajira kwa vijana ambao idadi yao ni zaidi ya asilimia 70 barani Afrika. 

“Tusaidiane kutatua changamoto za vijana barani Afrika kwa kuwa migogoro itakayosababishwa na vijana, nchi zitakazoathirika na migogoro hiyo sio Afrika pekee, bali hata Ulaya itaathirika kama inavyotokea katika baadhi ya nchi za Kaskazini mwa Afrika,” alisisitiza.